TETESI za kiungo wa Singida Black Stars, Clatous Chama, kurejea tena ndani ya kikosi cha Simba SC zimezidi kupamba moto, baada ya mchezaji huyo kutoa kauli fupi iliyozua mjadala mkubwa miongoni mwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi.
Chama aliibua hisia hizo kupitia majibu yake kwa shabiki mmoja aliyemkaribisha kurejea Simba, ambapo mchezaji huyo alijibu kwa maneno mawili tu, “Mapema tu”, kauli ambayo wengi wameitafsiri kama ishara ya wazi ya uwezekano wa kurejea kwake Msimbazi.
Katika kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili, jina la Chama limekuwa likihusishwa kwa nguvu na Simba, huku ikielezwa kuwa mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu Tanzania Bara wanatafuta kuimarisha safu ya kiungo kuelekea nusu ya pili ya msimu.
Mashabiki wa Simba wamekuwa mstari wa mbele kuonyesha mapenzi yao kwa mchezaji huyo kupitia mitandao ya kijamii, wakimiminika na jumbe za kumkaribisha nyumbani pamoja na kumuonesha imani kubwa waliyonayo juu ya uwezo wake.
Ujumbe mmoja uliovuta hisia za wengi ni ule wa shabiki aliyemwandikia Chama, “Karibu Msimbazi mwamba”, ambapo majibu ya haraka kutoka kwa mchezaji huyo yalitosha kuzua mjadala mpana miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka.
Kauli hiyo imeongeza matumaini kwa mashabiki wa Simba, ambao wanaamini kurejea kwa Chama kunaweza kuipa timu nguvu mpya, hasa katika mbio za mataji ya ndani na mashindano ya kimataifa.
Ikumbukwe kuwa Clatous Chama aliwahi kuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Simba SC katika misimu iliyopita, kabla ya kujiunga na Yanga SC, kisha kuhamia Singida Black Stars msimu huu, huku sasa jina lake likitajwa tena kwa nguvu kuhusishwa na kurejea Msimbazi.





