RABAT:SERIKALI ya Gabon imetangaza kuisimamisha kwa muda timu ya taifa, kumfuta kazi kocha pamoja na kuwaondoa kwenye kikosi wachezaji wakubwa akiwemo Pierre-Emerick Aubameyang, baada ya timu hiyo kufanya vibaya kwenye fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) zinazoendelea Morocco.
Tangazo hilo limetolewa na Waziri wa Michezo wa Gabon, Simplice-Desire Mamboula, kupitia televisheni ya taifa, baada ya Gabon kumaliza mkiani mwa Kundi F na kuaga mashindano mapema. Gabon ilipoteza mechi zake zote tatu, ya mwisho ikiwa ni kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Ivory Coast mjini Marrakech.
Waziri huyo amesema kutokana na kiwango duni kilichooneshwa na timu hiyo, serikali imeamua kulivunja benchi la ufundi, kusimamisha timu ya taifa hadi hapo itakapotangazwa vinginevyo, pamoja na kuwaondoa kwenye timu wachezaji Bruno Ecuele Manga na Pierre-Emerick Aubameyang.
Gabon, iliyokuwa chini ya kocha Thierry Mouyouma, ilikuwa tayari imeshaondolewa kwenye mashindano baada ya kupoteza mechi mbili za mwanzo dhidi ya Cameroon na Msumbiji. Kwenye mchezo wa mwisho dhidi ya Ivory Coast, Gabon walikuwa mbele kwa mabao 2-0 lakini wakaruhusu mabao matatu na kupoteza, tena dhidi ya kikosi cha pili cha mabingwa hao watetezi.

Aubameyang na beki mkongwe Ecuele Manga hawakushiriki mchezo huo wa mwisho. Aubameyang alirejea kwenye klabu yake ya Olympique de Marseille kwa matibabu ya jeraha la paja. Baada ya uamuzi wa serikali, Aubameyang alijibu kupitia mitandao ya kijamii akisema matatizo ya timu ya taifa ni makubwa zaidi kuliko kumlaumu mchezaji mmoja.
Kwa umri wa miaka 36, kuna uwezekano mkubwa kuwa Aubameyang tayari ameichezea Gabon mechi yake ya mwisho, hali iliyo sawa pia kwa Ecuele Manga mwenye miaka 37. Ingawa zamani kusimamishwa kwa timu za taifa kulikuwa jambo la kawaida barani Afrika baada ya matokeo mabaya, siku hizi ni nadra kutokana na FIFA kupinga vikali kuingiliwa kwa vyama vya soka na serikali.
The post Serikali ya Gabon yaisimamisha timu ya taifa first appeared on SpotiLEO.



