Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) jana zilipigwa mechi nne, lakini jioni ya leo kuna pambano la kukata na shoka baina ya mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo Simba Queens na JKT Queens zitakazonyeshana kazi.
Mechi hiyo inatarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kuanzia saa 12:00 jioni, huku timu hizo zikichuana katika msimamo wa ligi hiyo.
JKT Queens ambao ni watetezi wa ligi ikitwaa msimu uliopita ikifikisha taji la nne kama ilivyokuwa kwa Simba tangu kuanza kwa ligi hiyo mwaka 2016 inataka kuendeleza ubabe wao, wakati Simba Queens wanapambana kurejesha taji ambalo walilipoteza mbele ya mahasimu wao.
Rekodi za msimu uliopita zilipokutana Simba ilivuna pointi nne, ikitoa sare ya 1-1 nyumbani kabla ya kuondoka na ushindi wa mabao 4-3 ugenini Mbweni.
Hata hivyo, katika mechi za hivi karibuni, JKT Queens iliitandika Simba Queens mabao 2–1 katika fainali ya Ngao ya Jamii.
Simba ambayo takribani wachezaji wanaoanza ni wapya tofauti na JKT yenye wachezaji wa waliopo muda mrefu kikosini hapo, imeanza vizuri ikishinda mechi zote sita ikiwemo ya dabi ya Kariakoo dhidi ya Yanga Princess ikiichapa mabao 2-0.
Mfululizo wa matokeo mazuri kwa Simba ndio yanakwenda kuonyesha ugumu wa mechi hiyo kutokana na na matokeo ya mabingwa hao kwenye mechi sita ikishinda tano na kutoa sare ya 1-1 na Fountain Gate Princess.
Ni mechi nyingine ya kufungua mlango wa mapambano ya moja kwa moja kati ya simba wanaowania ubingwa na JKT Queens wanaolitetea, na matokeo yake yanaweza kuathiri msimamo wa kileleni.
Miongoni mwa wachezaji hatari ambao mabeki wa Simba wanapaswa kumchunga kwa umakini ni winga machachari, Winifrida Gerald mwenye mabao saba hadi sasa, amekuwa mwiba mchungu anapokutana na timu za Kariakoo kama sio kufunga basi anasababisha faulo au penati.
Mwingine ni mshambuliaji kinda, Jamila Rajabu ingawa hazungumzwi sana lakini mchezaji mwenye madhara makubwa anapopata mpira msimu huu tayari amefunga mabao matatu na kuhusika kwenye mabao matano.
Kwa upande wa Simba, Jentrix Shikangwa bila shaka ndiye mshambuliaji wa kigeni mwenye rekodi nzuri za kuwa na muendelezo wa kufunga, msimu wake wa kwanza 2021/22 aliweka kambani mabao 17 uliofuata nane na msimu jana 23 hadi sasa ana mabao matano.
Mwingine ni Aisha Mnunka msimu uliopita hakufanya vizuri lakini msimu huu tayari ameweka kambani mabao manne akiwa moja ya nguzo muhimu ya ushambuliaji kwa Wanamsimbazi hao.
Kocha msaidizi wa Simba, Mussa Mgosi alisema kuwa hana presha ya kukutana na mpinzani wake kwani msimu huu kila mechi ni fainali.
“Kwa upande wangu sina presha ya kukutana na JKT Queens kwa kuwa ninawafahamu vizuri na wao pia wanatufahamu hivyo tunapaswa Kuingia kwa tahadhari kubwa,” alisema Mgosi.
Kocha wa JKT, Kessy Abdallah alisema ni mechi wanayoichukulia kwa ukubwa wake akiamini maandalizi waliyoyafanya yatawapa matokeo.
“Si mchezo wa kudharau tunapaswa kujituma ili tuweze kupata matokeo mazuri tunaomba mashabiki wetu na watanzania wajitokeze kwa wingi hapo leo.”
The post SIMBA, JKT QUEENS VITANI WPL appeared first on Soka La Bongo.





