Hatua ya makundi ya Kombe la Mapinduzi 2026 imehitimishwa juzi Jumanne tukishuhudia vita ya Ligi Kuu Bara ikihamishiwa Unguja kwenye Uwanja wa New Amaan Complex pale Yanga ilipocheza dhidi ya TRA United.
Matokeo ya mechi hiyo ambapo Yanga imeshinda 1-0, yamekamilisha timu nne zitakazocheza nusu fainali leo Alhamisi na kesho Ijumaa uwanjani hapo, kisha Januari 13, 2026 fainali itapigwa kule Gombani kisiwani Pemba ambapo timu yoyote itakayokubali kupoteza inajua kabisa kwamba inang’oka michuanoni.
Nusu fainali ya kwanza inapigwa leo ikizikutanisha Simba na Azam FC katika pambano la Dabi ya Mzizima, mezi mmoja tu tangu zilipokutana katika Ligi Kuu msimu huu na Mnyama kupoteza kwa mabao 2-0.
Azam imetinga nusu fainali baada ya kuwa kinara wa kundi A ikimaliza na pointi saba baada ya kushinda mechi mbili dhidi ya Mlandege (2-0) na URA (2-1) na sare moja dhidi ya Singida Black Stars (1-1).
Kwa upande wa Simba, imemaliza kinara wa kundi B ikishinda mechi zote mbili ilizocheza dhidi ya Muembe Makumbi City (1-0) na Fufuni (2-1).
Rekodi zinaonyesha katika Kombe la Mapinduzi, timu hizi zimekutana mara saba tangu Azam FC ilipoanza kushiriki mwaka 2011.
Katika mechi hizo saba, hatua ya nusu fainali zimekutana mara tatu, mwaka 2012 ambapo Azam ilishinda 2-0, kisha mwaka 2013 Azam ikashinda kwa penalti 5-4 baada ya dakika tisini kuwa 2-2 na 2020 Simba ilishinda kwa penalti 3-2 baada ya muda wa kawaida matokeo kuwa 0-0.
Kwa ujumla, Azam imeshinda mechi tano dhidi ya mbili za Simba kwenye kombe la Mapinduzi.
Matokeo ya mechi hizo yapo hivi; Azam 2-0 Simba (nusu fainali 2012), Azam 2-2 Simba (Azam ikashinda kwa penalti 5-4 nusu fainali 2013), Azam 1-0 Simba (fainali 2017), Azam 1-0 Simba (makundi 2018), Azam 2-1 Simba (fainali 2019), Azam 0-0 Simba (Simba ikashinda kwa penalti 3-2 nusu fainali 2020) na Azam 0-1 Simba (fainali 2022).
Mara ya mwisho timu hizi zimekutana Desemba 7, 2025 katika Ligi Kuu Bara na Azam ikashinda 2-0 pale Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Safu ya ulinzi ya Simba ikiongozwa na Rushine De Reuck na Chamou Karaboue ambao walipumzishwa mechi iliyopita dhidi ya Fufuni, kutokana na ugumu wa mechi ya leo wanaweza kurudi kikosini.
Kikosi cha Simba kimepata nguvu baada ya kurejea kwa Jean Charles Ahoua na Jonathan Sowah ambao walikosekana mechi zote mbili za makundi, huku Elie Mpanzu akiiwahi moja iliyoipeleka Simba nusu fainali.
Azam ina mziki wake kamili, ukiachana na wale waliokuwa na kikosi cha Stars waliokwenda kushiriki AFCON akiwamo Feisal Salum, waliobaki ni watu wa kazi pia.
Jephte Kitambala anaongoza safu ya ushambuliaji huku akiwa miongoni mwa vinara wa mabao akifunga mawili.
Mshambuliaji huyu aliwaliza Simba mara ya mwisho walipokutana sambamba na Idd Nado ambaye anakosekana leo, lakini mpishi wa yale mabao ambayo Azam iliilaza Simba 2-0, Nassor Saadun yupo ndani ya nyumba licha ya kutocheza mechi hata moja ya Mapinduzi.
Kocha wa Simba, Steve Barker, amezungumzia mechi hiyo akisema ni kipimo kizuri kwake wakati huu akiwa anaijenga timu imara.
Kocha huyo Msauzi aliyetambulishwa kikosini hapo Desemba 19, 2025, hii ni mechi yake ya kwanza kukutana na Azam ambayo anafahamu mara ya mwisho Simba ililambishwa utamu ikiwa timu mwenyeji.
“Nafahamu tulipoteza mechi msimu huu dhidi ya Azam, kukutana na timu kubwa kama hii kipindi hiki kwangu inanipa motisha katika kujenga timu.
“Mechi hiyo itanipa picha ya kwamba tupo wapi hadi sasa katika maandalizi yetu kukabiliana na timu kubwa kama Azam kwa sababu tunafahamu mbele yetu tuna michezo mikubwa ya mashindano inakuja.
“Hata hivyo, ili tufanye vizuri lazima tucheze mchezo wa haraka, tuwe na mbinu bora zitakazorahisisha hiyo kazi.”
Kwa upande wa kocha wa Azam, Florent Ibenge, alisema: “Kila mechi imekuwa na changamoto yake, ukiangalia hatua ya makundi tumekutana na timu ngumu, sasa tunakwenda hatua ngumu zaidi kukutana na ushindani mwingine, tupo tayari kushindana tukiwa na malengo ya kubeba ubingwa na kuimarisha timu kuelekea mechi za CAF.”
The post UKIPIGWA UNAKWENDA KWENU appeared first on Soka La Bongo.





