KIUNGO mshambuliaji wa Yanga, Max Nzengeli, amemtaja mchezaji mwenzake Pacome Zouzoua kuwa ni mmoja wa wachezaji anaofanana naye zaidi uwanjani kutokana na uelewano mkubwa walioujenga ndani ya kikosi hicho.
Max alitoa kauli hiyo baada ya kuisaidia Yanga kufuzu kucheza fainali ya Kombe la Mapinduzi, kufuatia bao pekee alilofunga katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Singida Black Stars.
Bao hilo lilitokana na pasi safi aliyopokea kutoka kwa Pacome, jambo lililoonyesha wazi mshikamano wao.
Akizungumza kuhusu uhusiano wao uwanjani, Max amesema Pacome ni mchezaji bora zaidi kuwahi kucheza naye, wanaelewana kwa kiwango cha juu bila hata kuhitaji maelekezo mengi.
Amesema mara nyingi pasi anazopokea hutoka kwa Pacome, kama ilivyokuwa kwenye mchezo huo wa nusu fainali.
Max ameongeza kuwa uelewano wao hauishii hapo pekee, akitolea mfano mchezo wa awali dhidi ya KVZ ambapo Pacome alifunga bao kwa pasi iliyotoka kwake, hali inayoonesha muunganiko wao wa kiufundi ndani ya kikosi cha Yanga.
Kwa mujibu wa Max, ushirikiano wao umeongeza nguvu na ubora ndani ya timu, huku akiamini kuwa muunganiko huo ni faida kubwa kwa Yanga katika mashindano mbalimbali wanayoshiriki.
Akizungumzia kuelekea fainali ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Azam FC, Max amesema wao kama wachezaji wanaingia kila mechi kwa lengo la ushindi.
Hata hivyo, amesema wanatambua ugumu wa mchezo huo kutokana na ubora na ushindani mkubwa wa wapinzani wao.
The post NZENGELI PACHA WA PACOME NDANI YA JANGWANI appeared first on Soka La Bongo.




