DAR ES SALAAM: KLABU ya Simba SC imerejea rasmi katika uwanja wa mazoezi kuanza maandalizi ya mchezo muhimu wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance ya Tunisia, huku uongozi wa klabu hiyo ukiwataka mashabiki wake kuwa watulivu kuhusu masuala ya usajili.
Wekundu hao wametoka Zanzibar na kurejea Dar es Salaam tangu juzi walikokuwa wanashiriki michuano ya Mapinduzi ambako walitolewa hatua ya nusu fainali baada ya kufungwa na Azam FC bao 1-0.
Kwa mujibu wa taarifa ya Meneja Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally Dar es Salaam leo, kikosi hicho tayari kimeanza mazoezi kwa lengo la kujiweka sawa kuelekea mchezo huo wa Kundi D utakaochezwa ugenini nchini Tunisia Januari 23, mwaka huu.
“Kikosi chetu kimerejea katika uwanja wa mazoezi kujiandaa na mchezo dhidi ya Esperance,” alisema Ahmed Ally.
Katika hatua nyingine, Ally aligusia shauku kubwa iliyopo miongoni mwa mashabiki wa Simba kuhusu taarifa za usajili, akibainisha kuwa suala hilo linafanyiwa kazi kwa umakini mkubwa na viongozi wa klabu kwa kushirikiana na benchi la ufundi.
“Tunafahamu shauku kubwa ya Wana Simba kusikia taarifa za usajili za klabu yao, lakini nichukue nafasi hii kuwaomba wawe watulivu nyakati hizi ambazo viongozi wetu wanafanyia kazi mapendekezo ya benchi la ufundi,” aliongeza.
Wekundu hao wa Msimbazi awali walianza vibaya michezo yah atua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa kupoteza michezo miwili huenda baada ya mapumziko ya muda kidogo wakarejea kivingine kwani wanatarajia kufanya maboresho chini ya Kocha mpya Steven Barkar.
The post Simba yaanza maandalizi ya kuivaa Esperance first appeared on SpotiLEO.





