DAR ES SALAAM:MPIGANAJI wa ngumi za kulipwa nchini Tanzania, Hassan Mwakinyo, amesema kuwa baadhi ya mapromota wasio na uwezo wanamtazama kama bondia mwenye madai makubwa ya malipo kuliko wapiganaji wengine wote wa ngumi za kulipwa.
Kupitia ujumbe aliouchapisha leo, instagramu, Mwakinyo amesema mtazamo huo unatokana na ukweli kwamba hakujawahi kutokea bondia wa kiwango chake kwa miaka mingi, jambo linalomfanya aamini kuwa anastahili heshima na malipo makubwa zaidi ndani ya tasnia ya ngumi.
“Inawezekana ni kweli mapromota wasio na kitu wananiona kama bondia ninayetaka malipo makubwa kuliko wote waliowahi kutokea kwenye ‘industry’ ya ngumi kwa karne zote.
“Lakini pia ni kwa sababu hajatokea bondia kama mimi kwenye ngumi kwa karne zote. This is my time, 2026,” ameandika Mwakinyo.
Mwakinyo ameongeza kuwa anaamini maombi yake yako karibu kujibiwa, akiwataka mashabiki na Watanzania kuendelea kumuombea na kumuunga mkono katika safari yake ya ndondi.
“Yule mtoto dua yake iko karibu sana kujibiwa, kwa pamoja tuseme Amen.
“Leo na pochi yenye noti we huwezi shika, usinichoshe mimi ni boss, mechi kuisha,” ameongeza Mwakinyo.
Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa ngumi na mashabiki, wengi wakisubiri kuona kama mwaka 2026 utakuwa mwanzo wa enzi mpya kwa Hassan Mwakinyo ndani ya ulingo wa ndondi za kulipwa.
The post Hassan Mwakinyo: Hakuna Bondia wa kunizidi first appeared on SpotiLEO.





