MALLORCA:JÜRGEN Klopp ameweka wazi msimamo wake kuhusu tetesi zinazomhusisha na Real Madrid, akitumia nafasi hiyo kuzungumzia kwa kina zaidi kuondoka kwa Xabi Alonso ndani ya muda mfupi tangu ateuliwe.
Akizungumza na Sport Talk, Klopp amesema kuondoka kwa Alonso baada ya miezi sita tu ni ishara tosha kwamba kuna matatizo ndani ya Real Madrid, na si suala la kocha peke yake.
“Ukiangalia Xabi Alonso, ambaye kwa zaidi ya miaka miwili Leverkusen ameonesha ni kocha wa kipekee sana, halafu analazimika kuondoka Real Madrid miezi sita tu baadaye, hiyo inaonesha wazi kwamba mambo hayako sawa kwa asilimia mia moja ndani ya klabu,” amesema Klopp.
Kocha huyo wa zamani wa Liverpool ameongeza kuwa hali hiyo inaonesha jinsi ambavyo muda wa subira umeisha ndani ya klabu hiyo, na jinsi matarajio yalivyo makubwa kupita kiasi.
“Hii inaonesha kuwa hakuna tena muda. Matarajio ndani ya Real Madrid ni makubwa mno. Lakini kinachoendelea pale hakina uhusiano wowote na mimi, na wala hainihusu,” ameongeza.
Kauli hiyo ya Klopp imekuja wakati ambao Real Madrid wako kwenye kipindi cha mabadiliko makubwa, huku wakitafuta mwelekeo mpya baada ya kuondoka kwa Alonso na uteuzi wa Alvaro Arbeloa kama kocha mpya wa kikosi cha kwanza.
The post Kinachoendelea Bernabeu hakinihusu- Klopp first appeared on SpotiLEO.





