COMING to America ni moja ya filamu ambazo mpaka leo bado zinaangaliwa na watu wanacheka kama mara ya kwanza. Hii ni filamu ya vichekesho lakini ndani yake kuna ujumbe mzito kuhusu maisha, mapenzi na kutafuta uhuru wa kuwa wewe mwenyewe.
Filamu inamzungumzia Prince Akeem, mrithi wa ufalme wa nchi ya kubuni inayoitwa Zamunda barani Afrika. Akeem ana kila kitu, ana utajiri, ana heshima, ana kila anachotaka. Tatizo ni moja tu, kila kitu kimeshapangwa. Anatakiwa kuoa mwanamke aliyefundishwa maisha yake yote kuwa mke wa mfalme, bila kuuliza, bila kupinga, bila hata kumpenda kweli.

Akeem hapendi hayo maisha. Anataka mwanamke wa kawaida atakayempenda yeye kama yeye, si kwa sababu yeye ni mtoto wa mfalme. Ndipo anaamua kufanya kitu cha kushangaza. Anaacha ufalme, anaacha utajiri, halafu anasafiri kwenda Marekani, New York, kuanza maisha kama mtu wa kawaida kabisa.
Akiwa huko Queens, New York, Akeem na rafiki yake Semmi wanaanza kuishi kwenye nyumba ya kawaida, wanaajiriwa kwenye mgahawa wa chakula cha haraka, wanaanza maisha ya chini kabisa. Hapo ndipo vichekesho vinaanzia. Unaona prince anayesafishwa miguu, sasa anasafisha sakafu. Mtu aliyekuwa na kila kitu, sasa anahangaika na kodi, mabosi na majirani.
Wakati huo huo, Akeem anakutana na Lisa, msichana anayemfanya aanze kuielewa vizuri maana ya mapenzi ya kweli. Lakini tatizo ni moja, Lisa hamjui kuwa Akeem ni prince. Anamjua kama kijana wa kawaida anayetafuta maisha. Hapo ndipo filamu inacheza na siri, mapenzi na maamuzi magumu.

Coming to America ni filamu ya kuchekesha sana, lakini pia inaonesha mambo halisi. Inaonesha tofauti ya maisha ya utajiri kupita kiasi na maisha ya kawaida. Inaonesha pia kuwa pesa na cheo havinunui mapenzi ya kweli. Akeem anajifunza kuwa heshima ya kweli inatoka kwenye jinsi unavyowatendea watu, si unachomiliki.
Uigizaji wa Eddie Murphy hapa ni wa aina yake. Anaigiza zaidi ya mhusika mmoja, na kila mmoja anakufanya ucheke. Filamu imejaa matukio ya kukumbukwa, maneno yaliyobaki mitaani, na vichekesho ambavyo hata leo bado vinafanya kazi.
Kwa kifupi, Coming to America ni filamu ya kuangalia ukiwa unataka kucheka, lakini pia unataka kuona hadithi yenye maana. Ni filamu inayokuonesha kuwa wakati mwingine, ili umpate unachotaka kweli, lazima uache ulipozoea na uanze upya kama mtu wa kawaida.

Filamu hii iliongozwa na John Landis na ina mastaa wakubwa kama Eddie Murphy, Arsenio Hall, James Earl Jones na Shari Headley. Coming to America ilitengenezwa kwa bajeti ya takribani dola milioni 39 za Kimarekani, na ilipigwa sana duniani kote mpaka ikaingiza zaidi ya dola milioni 280. Mafanikio haya yaliifanya kuwa moja ya filamu kubwa zaidi za vichekesho za miaka ya 1980 na mpaka leo bado inaendelea kupendwa na kuangaliwa na vizazi tofauti.
Coming to America ilipokelewa vizuri na wakosoaji na mashabiki. Kwenye tovuti ya Rotten Tomatoes, filamu ilipata alama ya asilimia 73 za mapokezi mazuri, ikimaanisha wengi waliipenda. Metacritic wao waliipa alama ya kati, wakionesha kuwa maoni yalikuwa mchanganyiko, lakini jambo la kuvutia zaidi ni mashabiki. Kwa mujibu wa CinemaScore, watazamaji waliipa filamu alama ya “A”, ishara kuwa waliifurahia sana.
Mbali na mafanikio yake kwa watazamaji, filamu hii pia ilitambuliwa kimataifa. Iliwahi kuteuliwa kuwania tuzo mbili za Oscar, upande wa mavazi bora na make-up bora, hasa kwa kazi kubwa iliyofanywa kubadili sura za Eddie Murphy na Arsenio Hall waliocheza wahusika wengi tofauti ndani ya filamu moja.
Haya yote ndiyo yaliyofanya Coming to America ibaki kuwa filamu ya kukumbukwa mpaka leo, si kwa vicheko tu, bali pia kwa ubunifu, kazi kubwa ya uigizaji na alama yake kwenye historia ya filamu za vichekesho.
The post Coming to America:Eddie Murphy alituliza akili humu first appeared on SpotiLEO.






