KATIKA ulimwengu wa uigizaji, Rowan Atkinson, anayefahamika zaidi kama Mr. Bean, ameweka alama isiyofutika kupitia uhusika wake wa kipekee anayevaa koti la rangi ya kahawia na tai nyekundu, huku rafiki yake mkuu akiwa ni dubu wa mdoli anayeitwa Teddy.
Uigizaji wake ni wa kipekee na wa aina yake ambao unapendwa na watu wa rika zote, kuanzia watoto, watu wazima, mitaani hadi viongozi wakubwa serikalini, bila kuhitaji mkalimani wala maneno mengi.

Mr. Bean ameithibitishia dunia kuwa kicheko hakina lugha; ni lugha ya mwili tu na vitendo vingi vya kustaajabisha.
Katika safari yake ya sanaa, Rowan hakuishia tu kuchekesha watu mitaani, bali alipata heshima kubwa iliyofika hadi kwenye kasri la Malkia wa Uingereza kupitia nishani ya CBE.
Makabati yake yamejaa tuzo za kila aina, ikiwemo ile ya mwigizaji bora wa vichekesho na tuzo kubwa za kimataifa kama International Emmy.

Kuhusu ugumu wa kazi yake, Atkinson alieleza katika mahojiano na jarida la The Times kuwa ucheshi wa namna hii si mchezo mrahisi:
“Kuigiza ucheshi wa sura na mwili ni kazi ngumu na inayochosha sana kuliko watu wanavyofikiria. Ni kama mchezo wa sarakasi, lakini tofauti ni kwamba hapa unacheza na hisia za watu badala ya kamba.”
Ingawa asili yake ni Uingereza, soko la kazi za Mr. Bean limevuka mipaka kwa kiasi kikubwa sana, huko China, India, na nchi za Kiarabu zikiwa miongoni mwa maeneo yanayoongoza kwa kupenda kazi zake.
Hapa kwetu Afrika, kazi zake zimekuwa zikitazamwa na familia kwa vizazi vingi kwa sababu hazihitaji utafsiri wa lugha. Katika mahojiano yake maarufu na kipindi cha ABC News, Atkinson alifafanua kwanini mhusika huyu anakubalika kila kona ya dunia.

“Siri ya mafanikio ya Mr. Bean ni kwamba yeye ni mtoto mdogo aliyefungwa ndani ya mwili wa mwanaume mzima. Watoto wa kila taifa wanafanana, hivyo ndiyo maana kila mtu duniani anaweza kumwelewa na kucheka naye bila kuhitaji maneno,” alisema.
Pamoja na kuwa mbobezi sana mbele ya kamera, Rowan Atkinson ni mtu mwenye busara kubwa anapofungua kinywa chake. Katika maisha yake anaamini kuwa kila mtu anaweza kujiona ndani ya uhusika wake kwa sababu ya asili yake ya kitoto na uwezo wa kuwasiliana bila sauti.
Akizungumza na shirika la habari la BBC kuhusu uamuzi wake wa kutotumia maneno mengi, alisema: “Sihitaji maneno ili kuelezea hadithi. Nataka watu waone kile ninachokifanya, kwa sababu vitendo vina nguvu ya ajabu ya kuvunja vizuizi vya lugha ambavyo maneno hayawezi kuvivuka.”

Leo hii, tunapoangalia urithi wake, tunaona mzee ambaye amechagua kupumzika na kuacha uhusika huo ubaki kama kumbukumbu. Ingawa watoto wake wamechagua maisha ya faragha, jina la Mr. Bean halitafutika kamwe.
Kupitia kazi zake alizofanya zinazosambaa katika mitandao ya kijamii ,Rowan amewafundisha wasanii chipukizi kuwa wabunifu na kuzingatia nidhamu ya hali ya juu inayoweza kufanya jina la mwigizaji liishi milele.
Hakika, kazi zake zimewafundisha wengi ulimwenguni kuwa wakati mwingine, kimya kina sauti kubwa ya kicheko kuliko kelele zote za dunia.
The post Fahamu siri iliyojificha uchekeshaji wa Mr. Bean first appeared on SpotiLEO.






