MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, kesho wanashuka dimbani kuikabili Mashujaa FC katika mchezo muhimu wa ligi utakaochezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Mchezo huo unabeba uzito mkubwa kwa Yanga ambao wanahitaji pointi tatu ili kuendelea kujiimarisha katika mbio za ubingwa.
Kuelekea pambano hilo, kikosi cha Yanga kimekuwa katika maandalizi makini kikitambua ugumu wa mchezo huo.
Mashujaa FC imeonyesha uimara mkubwa msimu huu, hasa katika safu ya ulinzi, jambo linaloifanya mechi hiyo kuwa ya ushindani mkubwa.
Kuelekea mchezo, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Gocalves, amesema Mashujaa ni timu bora na yenye nidhamu ya hali ya juu uwanjani. katika mechi tisa walizocheza, Mashujaa wameruhusu mabao manne pekee, hali inayoashiria uimara wao katika kujilinda.
Gocalves amesisitiza kuwa kukutana na timu ya aina hiyo ni changamoto nzuri kwa Yanga, akieleza kuwa benchi la ufundi limejipanga vyema kuhakikisha wanacheza kwa umakini mkubwa huku wakifuata falsafa ya klabu hiyo ya kucheza soka la kuvutia na kushinda.
“Ni kweli Mashujaa ni timu nzuri, hata kwenye kushambulia. Tunatarajia mchezo mzuri, lakini kazi yetu ni kucheza vizuri na kushinda,” amesema kocha huyo.
Kocha huyo raia wa Ureno ametumia nafasi hiyo kuwaomba mashabiki wa Yanga, maarufu kama Wananchi, kujitokeza kwa wingi uwanjani kuisapoti timu yao.
Amesema sapoti yao imekuwa chachu kubwa ya mafanikio ya timu na anaamini uwepo wao kesho utawapa nguvu zaidi wachezaji.
“Nina furaha kubwa kila ninapowaona Wananchi uwanjani. Nawapongeza kwa sapoti yao ya dhati na nawaomba waje kutusapoti kesho dhidi ya Mashujaa. Nina imani watafurahi,” alimalizia Gocalves kwa matumaini makubwa.
The post YANGA NDANI YA POINT TATU DHIDI YA MASHUJAA appeared first on Soka La Bongo.






