DAR ES SALAAM:MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Barnaba Elias maarufu kama Barnaba Classic, ametoa ujumbe mzito kwa watu wanaojitambulisha kuwa ni marafiki au watu wake wa karibu, akiwataka kupunguza mazoea na kulinda heshima katika mahusiano yao.
Barnaba ameeleza hayo kupitia Insta Story yake, akisisitiza kuwa kuzoeana hakupaswi kuwa sababu ya kudharau heshima, hadhi na misingi waliyoijenga kwa muda mrefu.
“Nataka kuwakumbusha mnaojita washkaji zangu au watu wangu wa karibu; kujuana kusiwe sababu ya kupotezeana heshima. Hadhi na nafasi tulizojenga kwa muda mrefu ni muhimu sana.Heshima ifuate mkondo wake na nidhamu izingatiwe siku zote,” ameandika Barnaba.
Barnaba huyo ameongeza kuwa mazoea yakizidi, hupelekea kupotea kwa utiifu na watu kuchukuliana poa kupita kiasi, jambo ambalo haliko tayari kulivumilia kuanzia mwaka huu wa 2026.
“Mazoea yakizidi, upoteza utiifu na kuchukuliana poa. Mwaka huu 2026 tutatiana ‘block’ kweli kweli, sio kwenye simu tu, hadi kazini,” ameongeza.
Barnaba pia ameweka wazi msimamo wake kuhusu kuheshimiana, akisema heshima ni ya pande zote na kila mmoja anatakiwa kujitambua.
“Asilimia moja nikikuheshimu, jiheshimu. Fuata misingi yangu. Ukiona huwezi, sema, nami nitatii kabisa. Hili liwaendee wale ambao mkiulizwa kuhusu sisi mnasema ‘hana shida nammudu’. Ole wako ujichanganye. Respect my condition always,” amehitimisha.
Ujumbe huo umeibua mjadala mpana mitandaoni, ambapo mashabiki na wadau wa burudani wameonekana kuunga mkono msimamo wa Barnaba, wakisema heshima ni msingi muhimu hata kwenye urafiki wa muda mrefu.
The post “Mimi sio wa mazoea!”-Barnaba Classic aweka msimamo mkali first appeared on SpotiLEO.





