MSHAMBULIAJI raia wa Ivory Coast, Jean Charles Ahoua, ameaga rasmi klabu ya Simba SC kwa kuacha ujumbe mzito uliojaa shukrani, heshima na kumbukumbu nzuri baada ya safari yake ndani ya kikosi hicho kufikia tamati.
Kupitia ujumbe wake alioutoa kwenye mitandao ya kijamii, Ahoua amesema safari yake Simba itabaki milele kwenye kumbukumbu zake, akieleza furaha na fahari aliyopata kuvaa jezi nyekundu na nyeupe ya klabu hiyo kongwe nchini Tanzania.
Ahoua hakusita kutoa shukrani zake kwa uongozi wa klabu, benchi la ufundi pamoja na wachezaji wenzake, akisema walimpa upendo, imani na ushirikiano mkubwa uliomsaidia kukua ndani na nje ya uwanja.
Pia aliwapongeza mashabiki wa Simba kwa sapoti kubwa waliyoonesha kwake katika kipindi chote alichokuwepo, akisisitiza kuwa mchango wao ulikuwa chachu ya mafanikio na kumbukumbu zisizosahaulika.
“Ninajivunia sana kuvaa jezi hii. Sura inayofuata ya maisha yangu ya soka itaandikwa kwingine, lakini heshima na mapenzi niliyopata Simba yataendelea kubaki moyoni mwangu,” amesema Ahoua katika ujumbe wake.
Kuondoka kwa Ahoua kunafungua ukurasa mpya kwa mchezaji huyo na klabu ya Simba SC, huku mashabiki wengi wakimtakia kila la heri katika safari yake mpya ya soka nje ya Tanzania.
The post UJUMBE MZITO WAACHWA NA AHOUA SIMBA SC appeared first on Soka La Bongo.





