BAADA ya kupoteza mchezo wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly nchini Misri, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema anaridhishwa na namna timu yake inavyoendelea kukua na kuonyesha ushindani katika michuano mikubwa.
Pedro amesema kupoteza dhidi ya Al Ahly si jambo la kushangaza, akieleza kuwa wamecheza dhidi ya timu kubwa yenye uzoefu mkubwa na historia ndefu ya kutwaa ubingwa mara kadhaa katika mashindano hayo ya kimataifa.
Ameongeza kuwa pamoja na matokeo hayo, benchi la ufundi limejifunza mengi kutokana na mchezo huo na tayari limeanza kujipanga kwa ajili ya mechi ijayo ili kurekebisha mapungufu yaliyojitokeza.
Yanga sasa wanarejea nyumbani kuendelea na maandalizi ya mchezo wa marudiano dhidi ya Al Ahly, utakaochezwa Januari 31, 2026 katika Uwanja wa New Amaan Complex, visiwani Zanzibar, huku matarajio yakiwa ni kufanya vizuri mbele ya mashabiki wao.
Katika mchezo wa awali, Yanga ilikubali kipigo cha mabao 2-0 dhidi ya wenyeji wao Al Ahly, lakini Pedro anaamini matokeo hayo hayapunguzi dhamira ya timu yake kupambana hadi dakika ya mwisho.
“Timu inakuwa, tumepoteza lakini kesho ni siku nyingine. Tunapaswa kurejea katika ari yetu ya kupambana na kutafuta matokeo mazuri katika mchezo wa marudiano,” amesema Pedro
The post PEDRO AJIVUNIA YANGA LICHA YA KIPIGO MISRI appeared first on Soka La Bongo.






