MENEJA wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, ameweka wazi sababu zilizopelekea kikosi cha timu hiyo kukosa nafasi ya kufanya mazoezi ya mwisho katika uwanja utakaotumika kwa mechi, akisema hatua hiyo ilitokana na maelekezo ya wasimamizi wa mchezo.
Simba inashuka dimbani leo ugenini kuivaa Esperance Sportive de Tunis katika mchezo wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, ikisaka ushindi wake wa kwanza katika hatua hiyo ya mashindano.
Akizungumza kuelekea mchezo huo, Ahmed amesema kikosi cha Simba kipo tayari kikamilifu na kimejipanga kupambana kwa nguvu zote licha ya changamoto zilizojitokeza kabla ya mechi.
“Hatukupata nafasi ya kufanya mazoezi katika uwanja ambao tunakwenda kuchezea, hali ambayo imetokana na maelekezo tuliyopokea kutoka kwa wasimamizi wa uwanja,” amesema Ahmed.
Amefafanua kuwa uwanja huo haukuwa katika hali nzuri kufuatia mvua kubwa iliyonyesha juzi na kusababisha mafuriko, sambamba na kutumika hivi karibuni kwenye mchezo wa dabi, wakaelekezwa kutoutumia kwa mazoezi ili kuupa muda wa kukauka.
Ahmed ameongeza kuwa hata wenyeji wao Esperance hawakuruhusiwa kufanya mazoezi katika uwanja huo, na badala yake walielekezwa kutumia viwanja vingine kwa ajili ya maandalizi ya mwisho kabla ya mchezo.
Kwa upande mwingine, amesema benchi la ufundi la Simba limefanya kazi kubwa kuwaandaa wachezaji kimbinu na kisaikolojia, jambo linalowapa imani ya kukabiliana na mazingira yoyote watakayokutana nayo uwanjani.
Amesema kusema Simba imezoea changamoto za aina hiyo inapocheza mechi za ugenini, na uzoefu huo utawasaidia wachezaji kuingia uwanjani wakiwa na umakini mkubwa na morali ya juu.
The post SIMBA YAWEKA WAZI SABABU YA KUKOSA MAZOEZI appeared first on Soka La Bongo.





