BAADA ya klabu ya Simba SC kumtambulisha rasmi kiungo mshambuliaji Iñno Jospin Loemba, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, amesema ujio wa mchezaji huyo ni sehemu ya dhamira ya klabu kuendelea kujiimarisha na kujijenga katika viwango vya juu zaidi vya ushindani.
Simba imemalizana na Loemba katika dirisha dogo la usajili, ikimtaja kama mmoja wa wachezaji waliolengwa kuongeza nguvu na ubora ndani ya kikosi, hususan katika safu ya kiungo na ushambuliaji, kuelekea mechi ngumu za Ligi Kuu Tanzania Bara na mashindano ya kimataifa.
Baada ya kumtambulisha nyota huyo, Ahmed Ally ametumia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii kuandika kuwa usajili wa Loemba unaonyesha namna Simba inavyovutia wachezaji wenye wasifu mkubwa, hali inayoongeza hadhi ya klabu ndani na nje ya nchi.
Amesisitiza kuwa uwepo wa wachezaji wa aina hiyo unaifanya Simba kuonekana zaidi katika macho ya dunia ya soka.
“Kwa kupata mchezaji wa kiwango hiki, unaweza hata kupata fursa ya kucheza mechi za kirafiki na klabu kubwa duniani kama Manchester United ili kujipima ubavu,” Ahmed Ally, akieleza matarajio makubwa ya klabu hiyo.
Kauli hiyo imezua mjadala miongoni mwa mashabiki wa Simba, wengi wao wakiona ni ishara ya malengo mapya na ndoto kubwa zinazowekwa na uongozi wa klabu, sambamba na juhudi za kuifanya Simba iwe klabu ya mfano barani Afrika.
Kwa ujumla, ujio wa Loemba umeongeza ari na matumaini mapya kwa Wanasimba, huku uongozi ukiendelea kusisitiza kuwa usajili wanaoufanya una lengo la kuipeleka klabu katika hatua nyingine ya mafanikio na ushindani wa kimataifa.
The post LOEMBA AICHOCHEA NDOTO YA SIMBA MAN UNITED appeared first on Soka La Bongo.





