KLABU ya Simba imeendelea kuvuna matunda ya mipango yake ya usajili baada ya kufanikiwa kumnasa kiungo mshambuliaji, Inno Jospin Loemba, hatua ambayo imeelezwa kuwa ni ushindi mkubwa kwa Wekundu wa Msimbazi katika dirisha hili.
Akizungumza kuhusu dili hilo, mzabuni wa Simba, Joseph Rwegasira, amesema usajili wa Loemba umezingatia mahitaji ya sasa ya klabu, huku benchi la ufundi likimtazama mchezaji huyo kama chaguo sahihi kutokana na uwezo, umahiri na ubora wake uwanjani.
Rwegasira amesisitiza kuwa Loemba ni mchezaji wa kiwango cha juu ambaye mchango wake utaonekana wazi pindi atakapoanza kutumika, akiamini kuwa Wanasimba watafurahia kile atakachokionesha ndani ya uwanja.
“Kwa sasa huyo mchezaji tumelamba dume. Mimi na Simba tupo pamoja katika kila jambo, kuna mengi ambayo tunafanya kwa maslahi ya klabu,” amesema Rwegasira akionyesha mshikamano wake na uongozi wa Simba.
Aidha, alifichua kuwa usajili wa Loemba haukuwa mwepesi, kwani kulikuwa na klabu nyingi zilizokuwa zikihitaji huduma ya nyota huyo, hali iliyosababisha ushindani mkali katika mchakato wa kumnasa.
Hata hivyo, Simba ilipambana kwa nguvu zote kuhakikisha inapata saini ya Loemba, jambo linaloonyesha dhamira ya klabu hiyo kuendelea kujijenga kikosi imara chenye uwezo wa kupambana katika mashindano ya ndani na kimataifa.
The post SIMBA KWA LOEMBA IMERAMBA DUME, JAYRUTTY appeared first on Soka La Bongo.




