BEKI wa Simba SC, Nickson Kibabage, amesema ana deni kubwa kwa mashabiki wa klabu hiyo baada ya baadhi ya watu kuubeza usajili wake tangu alipojiunga na wekundu hao wa Msimbazi.
Kibabage alijiunga na Simba katika dirisha dogo la usajili akitokea Singida Black, hatua iliyolenga kuongeza nguvu na ushindani katika safu ya ulinzi ya kikosi hicho kinachoshiriki mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Akizungumza kuhusu changamoto na matarajio yake, Kibabage amesema kuwa maneno ya kubezwa hayakumkatisha tamaa bali yamekuwa chachu ya kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kuthibitisha uwezo wake ndani ya uwanja.
“Nina deni kwa Simba. Kuna watu walikuwa hawaamini usajili wangu hasa wakati wa utambulisho. Hilo linanifanya nipambane zaidi, nijitume na kuwaonyesha kwamba inawezekana tukafanya kitu kikubwa ndani ya klabu ya Simba,” amesema Kibabage.
Beki huyo amesema ana imani kubwa na kikosi cha Simba kutokana na mshikamano uliopo miongoni mwa wachezaji, akisisitiza kuwa umoja na upendo ndiyo silaha muhimu ya mafanikio ya timu hiyo.
Ameongeza kuwa anaendelea kujifunza, kufanya kazi kwa bidii mazoezini na kusubiri nafasi yake ili kutoa mchango chanya pale atakapopata nafasi ya kucheza, akiahidi kupambana kwa ajili ya heshima ya jezi ya Simba na kuwalipa wanasimba deni alilonalo.
The post NINA DENI KWA WANA SIMBA, KIBABAGE appeared first on Soka La Bongo.





