SIMBA SC imeshindwa kufanikisha dhamira yao ya kupata alama tatu nyumbani baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 dhidi ya Esperance de Tunis katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Simba ilianza mchezo kwa kasi na nidhamu kubwa, hali iliyowawezesha kupata bao la kwanza dakika ya 38 kupitia beki Shomari Kapombe aliyechukua jukumu la mkwaju wa penalti na kupiga kwa utulivu kabla ya kuitikisa nyavu za wageni hao kutoka Tunisia.
Dakika chache kabla ya mapumziko, Simba waliongeza bao la pili kupitia Kagoma aliyefunga dakika ya 45, na kuifanya timu hiyo kwenda mapumzikoni ikiwa kifua mbele kwa mabao 2-0 huku mashabiki wakiamini ushindi mnono upo njiani.
Hata hivyo, kipindi cha pili kilishuhudia mabadiliko makubwa baada ya Esperance kurejea kwa nguvu. Aboubacar Diakité aliipatia timu yake bao la kwanza dakika ya 63, kabla ya Kouceila Boualia kusawazisha bao la pili dakika ya 79 na kuifanya mechi kumalizika kwa sare ya 2-2.
Matokeo hayo yameifanya Simba kuvuna alama moja pekee nyumbani na kujiweka katika mazingira magumu ya kusonga mbele kuelekea hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo kuendelea kuhitaji matokeo ya miujiza katika michezo ijayo ya kimataifa.
The post SIMBA YAENDELEA KUOMBA MUNGU KIMATAIFA appeared first on Soka La Bongo.






