ALIYEKUWA kiungo wa Klabu ya Simba, Jean Charles Ahoua ambaye kwa sasa anakipiga katika klabu ya CR Belouizdad ya Algeria, tayari yupo nchini kwa ajili ya mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Singida Black Stars utakaochezwa visiwani Zanzibar.
Nyota huyo aliyewahi kuichezea Simba aliuuzwa kwenda CR Belouizdad, klabu ambayo Jumapili, Februari 8, 2026 itakuwa mgeni katika dimba la New Amaan Complex, Zanzibar, ikisaka matokeo mazuri ugenini.
Ahoua ameonekana kuwa katika kiwango bora wakati wa mazoezi ya mwisho ya timu hiyo, akionyesha umakini mkubwa, nguvu na ari ya kupambana, hali inayotoa matumaini makubwa kwa benchi la ufundi la CR Belouizdad kuelekea pambano hilo muhimu.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya kambi ya timu hiyo, kiungo huyo ameweka wazi kuwa yupo tayari kupambana kwa dakika zote, akisisitiza kuwa mchezo huo ni muhimu kwao katika kuhakikisha wanapata matokeo chanya ugenini.
CR Belouizdad inatarajia kutumia uzoefu wa Ahoua katika eneo la kati, hasa katika kudhibiti kasi ya mchezo, kusambaza mipira na kusaidia safu ya ushambuliaji dhidi ya Singida Black Stars.
Kwa upande wao, Singida Black Stars wanaingia kwenye mchezo huo wakiwa na hamasa kubwa, wakilenga kutumia faida ya uwanja wa nyumbani na sapoti ya mashabiki wao kuhakikisha wanapata ushindi muhimu.
Pambano hilo kati ya CR Belouizdad na Singida Black Stars linatajwa kuwa miongoni mwa mechi zinazovutia zaidi wikendi hii, huku macho mengi yakielekezwa kwa Jean Ahoua kuona kama ataonyesha makali yake ndani ya uwanja wa New Amaan Complex.
The post AHOUA AREJEA TANZANIA, MOTO CAF WAWAKA ZANZIBAR appeared first on Soka La Bongo.





