WAKATI baadhi ya Wanasimba wakianza kukata tamaa na kuona safari ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika imefikia tamati, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, ameibuka na kauli nzito akiahidi kuharibu furaha ya wapinzani wao Petro de Luanda katika mchezo wa marudiano.
Simba wanatarajiwa kushuka dimbani wakiwa na morali ya juu, si kwa unyonge, wakilenga kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo wao wa kesho dhidi ya wenyeji wao Petro de Luanda utakaochezwa nchini Angola.
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo, Barker amesema kikosi chake kimejipanga kikamilifu na maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa kuzingatia ugumu na ushindani mkubwa wa mchezo huo wa kimataifa.
Kocha huyo amesema benchi la ufundi linaelewa presha iliyopo, lakini badala ya kuwavuruga, presha hiyo imeongeza ari na umakini kwa wachezaji. Amefafanua kuwa kila mchezaji anafahamu majukumu yake pamoja na malengo ya timu ndani ya uwanja.
“Lengo kubwa la Simba katika mchezo wa kesho ni kuonyesha soka bora linaloendana na hadhi ya klabu. Kushinda na kupata pointi tatu ni muhimu, lakini si kwa gharama ya kupoteza mpangilio wa timu,” amesema Barker.
Ameongeza kuwa maandalizi yote yako tayari na namna walivyojipanga inawapa imani ya kuonyesha mchezo mzuri na kupigania ushindi, huku akitambua wazi ugumu wa pambano hilo.
Barker amesema Petro de Luanda ni timu yenye uwezo mkubwa, jambo lililowafanya kufanya tathmini ya kina ya mbinu za wapinzani wao. Ameweka wazi kuwa Simba haitaingia uwanjani kwa kubeza yeyote, bali kwa heshima kubwa na umakini wa hali ya juu.
kocha huyo amewapongeza wachezaji wake kwa nidhamu na morali waliyonayo kambini, akisisitiza kuwa hali hiyo imeongeza imani kuwa timu iko tayari kimwili na kiakili kwa pambano la kesho.
The post BARKER ASUKA MPANGO MZITO, SIMBA KUINGIA VITANI appeared first on Soka La Bongo.






