KIKOSI cha Yanga kinatarajiwa kushuka dimbani kesho jijini Rabat, Morocco, katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS FAR Rabat, pambano lenye uzito mkubwa kwa hatma ya timu hiyo katika michuano hiyo ya kimataifa.
Katika mchezo huo muhimu, Yanga inahitaji ushindi au sare ili kujihakikishia tiketi ya kusonga mbele na kufuzu hatua ya robo fainali, hali inayofanya presha kuwa kubwa kwa pande zote mbili kuelekea dakika 90 za maamuzi.
Kuelekea pambano hilo, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves, amesema wanaifahamu vyema AS FAR Rabat kama timu imara yenye uwezo wa kubadilika kimbinu kulingana na mazingira ya mchezo na mahitaji ya wakati husika.
Pedro amesema maandalizi ya kikosi chake yamezingatia uwezekano wa aina mbalimbali za mchezo kutoka kwa wapinzani wao, akisisitiza kuwa lengo kuu ni kutimiza dhamira waliyoifuata nchini Morocco.
“Hakuna timu bora isiyo na mapungufu. Tumefanya tathmini ya kina ili kutumia madhaifu yao kupata matokeo tunayoyahitaji. Tuna kikosi chenye ubora wa kukabiliana na mazingira magumu pamoja na presha ya mechi kubwa,” amesema Pedro.
Kocha huyo ameongeza kuwa timu imekuwa na maandalizi mazuri na mwendelezo chanya wa kutengeneza nafasi katika michezo yao ya hivi karibuni, akieleza imani yake kuwa kesho wataendelea kucheza kwa kasi na umakini.
“Tunaheshimu wapinzani wetu, wana kikosi kizuri kuanzia safu ya ulinzi hadi ushambuliaji na ni moja ya klabu kubwa hapa Morocco. Hata hivyo, tunaamini tuna nafasi ya kufanya vizuri na tunapaswa kutumia nafasi zetu kwa umakini mkubwa,” ameongeza.
Pedro amesema ana imani kubwa na wachezaji wake kutokana na maandalizi ya kimbinu pamoja na utayari wao wa kiakili kupambana hadi dakika ya mwisho ya mchezo.
Hata hivyo, kocha huyo ameonyesha masikitiko yake juu ya mchezo huo kuchezwa bila uwepo wa mashabiki uwanjani, akieleza kuwa hali hiyo inapunguza ladha halisi ya mchezo wa soka.
“Sina furaha kucheza bila mashabiki. Mpira wa miguu ni kwa ajili ya mashabiki na ni vigumu kuwa na furaha ya kuburudisha watu ambao hawapo uwanjani,” amesema.
Pedro ameonyesha matumaini kuwa matukio ya michezo kuchezwa bila mashabiki hayatakuwa jambo la kawaida tena katika soka la Afrika, akisisitiza umuhimu wa wadau wote kuutunza na kuuheshimu mchezo huo.
The post BILA MASHABIKI, YANGA KUISHTUA FAR RABAT appeared first on Soka La Bongo.





