ZANZIBAR : MWANAMUZI mkongwe Salif Keita ameshindwa kufika Zanzibar na kutumbuiza katika Tamasha la Sauti za Busara 2026 kutokana na kuugua.
Mkurugenzi wa Tamasha hilo, Journey Ramadhani amesema taarifa ya kuugua kwa mwanamuziki huyo aliyekuwa akitarajiwa kutumbuiza siku ya mwisho ya tamasha hilo wameipokea kutoka kwa mwanamuziki huyo baada ya kushauriwa na daktari wake kutosafiri kutokana na afya yake kutokuwa sawa.
“Tumepokea taarifa ya mwanamuziki huyo kutopanda jukwaani baada ya kushauriwa na daktari wake, awali mwanamuziki huyo alitaka kuja na bendi yake lakini daktari wake alimshauri asisafiri ili kulinda afya yake,” alieleza Journey.
Journey amesema kukosekana kwa Salif Keita katika burudani ya Tamasha hilo hakujaathiri tamasha hilo kutokana na bendi yake iliyojaa wanamuziki wenye weredi na uwezo mkubwa wa kuimba nyimbo zake zote maarufu na kutumia vyombo mbalimbali walifika na kukonga nyoyo za mashabiki waliofurika katika viwanja vya Mnazi Moja visiwani hapa.
Baada ya kumaliza onesho lao na wimbo wa Africa majira ya saa 7 usiku wasanii hao hawakuzungumza na waandishi wa Habari bali walielekea moja kwa moja Uwanja wa ndege wa Abeid Karume Zanzibar na kurejea nchini Mali kuungana na ndugu yao huku wakiwaacha mashabiki wao wakitamani shoo iendelee.
The post Ugonjwa wamfanya Salif Keita ashindwe kutumbuiza Sauti za Busara 2026 first appeared on SpotiLEO.




