KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steven Barker, amesema kikosi chake kina hamasa kubwa ya kurejea kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kumaliza ratiba ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF), amesisitiza kuwa sasa nguvu zao zote zinaelekezwa kwenye mashindano ya ndani.
Barker amesema tayari Simba imerejea mazoezini kujiandaa na mchezo dhidi ya KMC utakaochezwa kesho jioni, huku akibainisha kuwa kila mchezo wa ligi una umuhimu mkubwa, hasa ikizingatiwa hali ya msimamo wa ligi kwa sasa.
Amesema Simba bado ina idadi ndogo ya mechi ikilinganishwa na baadhi ya wapinzani wake, jambo linalowalazimu kupambana kuhakikisha wanapata pointi tatu katika kila mchezo ili kuendelea kubaki karibu na kilele cha msimamo wa Ligi Kuu.
“Kwa sasa tuko nyuma kwa idadi ya mechi tulizocheza ukilinganisha na wapinzani wetu, hivyo ni muhimu kuhakikisha tunapata pointi zote tatu ili kuendelea kusalia karibu na kilele cha msimamo wa ligi,” amesema Barker.
Kocha huyo ameongeza kuwa licha ya kuwaheshimu wapinzani wao, anatambua hakuna mchezo mwepesi katika Ligi Kuu, huku akifurahishwa na kiwango cha kujituma na nidhamu kinachoendelea kuoneshwa na wachezaji wake katika mazoezi na michezo ya hivi karibuni.
“Ninaamini timu inaendelea kukua kutoka mchezo mmoja hadi mwingine. Tunazidi kuwa imara, na kama baadhi ya viwango tulivyovionesha hivi karibuni vitaendelea kudumishwa, tayari tumeweka msingi mzuri kwa mafanikio ya baadaye,” amesema.
Barker amesema wachezaji wapya waliotua ndani ya kikosi wameanza kuzoea mazingira ya timu na kuungana vizuri na wenzao, hali inayowapa Simba mwelekeo mzuri na kasi mpya (momentum), hasa baada ya kupitia mechi ngumu za Ligi ya Mabingwa Afrika.
Amesema benchi la ufundi linaangalia mbele kwa matumaini makubwa, likisubiri kwa hamu mchezo wa kesho wa Ligi Kuu kama mwanzo mpya wa safari yao ya kurejesha makali katika mashindano ya ndani.
The post BARKER AFICHUA SIRI KUONGEZA KASI BAADA YA CAF appeared first on Soka La Bongo.



