DAR ES SALAAM: KOCHA Miguel Gamondi amesaini mkataba rasmi wa kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kwa mkataba wa miaka miwili.
Hafla ya utiaji saini wa mkataba huo imefanyika leo, Februari 16, 2026, katika Uwanja wa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia, pamoja na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Paul Makonda amesema kuwa Gamondi amestahili kupewa mkataba huo baada ya kuonesha uwezo mkubwa katika michuano ya Mataifa ya Afrika 2025 (AFCON 2025) iliyofanyika nchini Morocco, ambapo aliiongoza Taifa Stars kufikia hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza akiwa kocha wa muda, hivyo kutokana na mafanikio hayo, Serikali imeamua kumwajiri rasmi ili aiongoze timu hiyo katika maandalizi ya mashindano ya AFCON 2027, ambayo Tanzania itakuwa mwenyeji.

Aidha, Waziri Makonda amesema Serikali imetoa kibali kwa kocha huyo kumchagua mchezaji yeyote wa Kitanzania anayecheza nje ya nchi ili kujiunga na timu ya taifa, ambapo ameongeza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kuendelea kuwekeza katika soka kwa lengo la kutimiza ndoto za vijana wengi wenye vipaji.

“Matarajio ya Dk. Samia ni kuhakikisha timu hii inakuwa bora zaidi na inapanda viwango, si tu katika ngazi ya CAF bali pia FIFA. Hivyo, Gamondi ana kazi kubwa ya kufanya. Maelekezo ya Dk. Samia ni kwamba kama kuna kijana yeyote wa Kitanzania popote duniani, aje alipiganie Taifa lake,” amesema Makonda.
Kwa upande wake, Kocha Miguel Gamondi ameishukuru Serikali kwa imani waliyoonesha kwake na kuahidi kufanya kazi kwa bidii, huku akisema kwamba ana imani kuwa kupitia ushirikiano kati ya Serikali na TFF, Tanzania inaweza kuwekwa kwenye ramani ya soka la Afrika.
“Nina furaha kubwa na ninajivunia kuwa Kocha wa Timu ya Taifa kwa miaka miwili ijayo. Ninaipenda Tanzania na ninaamini tunaweza kufanya jambo la kipekee. Ninaahidi kufanya kazi kwa bidii, kuwa na imani, na kujitahidi kuifurahisha nchi nzima,” amesema Gamondi.

Naye Rais wa TFF, Wallace Karia, amesema Shirikisho litaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mpira wa miguu nchini unafanya vizuri zaidi, kwa lengo la kuitangaza Tanzania kimataifa na kuwaletea furaha Watanzania.
The post Kazi mnayo, Gamondi apewa stars mazima! first appeared on SpotiLEO.




