DAR ES SALAAM: WASANII wa Filamu za Bongo Movie nchini, Rihama Ally na Shamila Rashid maarufu kama Bi Staa, wamekutanishwa katika filamu mpya ya Koti Jeupe inayotarajiwa kuzinduliwa Februari 17, 2026 katika ukumbi wa Dar Free Market, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Spoti leo jijini, Mwongozaji na mwandishi wa filamu hiyo, Sylvia Lyimo, amesema kuwa kazi hiyo imelenga kuonesha umuhimu wa bima ya afya na maisha, hususan namna inavyoweza kuwa kinga na msaada kwa familia pindi zinapokumbwa na majanga.
“Katika filamu hii kuna binti anayejulikana kwa jina la Amanda ambaye amelelewa katika maisha bora na wazazi wake, Riyama na Ben Selengo. Hata hivyo, hali inabadilika ghafla baada ya baba yake kupoteza maisha,” amesema Lyimo.
Ameeleza kuwa tukio hilo linabadilisha kabisa mwelekeo wa maisha ya Amanda, anayelazimika kuishi kwa mjomba wake mwenye mienendo isiyofaa. Hali hiyo inaathiri ustawi wake na ndoto zake za kuendelea na masomo.
Filamu hiyo imeakisi uhalisia wa maisha ya baadhi ya mabinti wa Kitanzania wanaokumbana na changamoto za malezi na kukosa ulinzi wa kutosha kutoka kwa jamii inayowazunguka.
Kwa upande wake, Bi Staa ambaye amecheza nafasi ya rafiki wa mama Amanda, amesema kupitia mhusika wake ameonesha umuhimu wa kuhamasisha elimu kwa watoto wa kike hata wanapokumbana na misukosuko ya maisha.
“Malezi ya siku hizi yamebadilika sana tofauti na zamani. Zamani mtoto wa mwenzako alikuwa ni wako, lakini sasa huwezi hata kumkanya mtoto wa jirani bila kuonekana umevuka mipaka,” amesema Bi Staa.
Ameongeza kuwa zamani mtoto angeweza kula kwa jirani na mzazi wake akapokea kwa moyo mkunjufu, lakini kwa sasa hali imebadilika kutokana na hofu na mabadiliko ya kijamii.
Naye Abdul Salum maarufu kama Ben Selengo, amecheza nafasi ya baba anayejitahidi kuhakikisha mwanae anapata elimu na maisha bora, licha ya changamoto zinazoikumba familia yake.
Kwa upande wake, mwigizaji aliyecheza nafasi ya Amanda ametoa rai kwa jamii kuishi kwa uangalifu na kuwajali watoto, hususan mabinti, ili waweze kutimiza ndoto zao badala ya kukatishwa tamaa na mazingira yasiyo rafiki.
Filamu ya Koti Jeupe inatarajiwa kugusa maisha halisi ya Watanzania na kuchochea mjadala mpana kuhusu malezi, uwajibikaji wa jamii pamoja na umuhimu wa mipango madhubuti ya kulinda mustakabali wa watoto.
The post KOTI JEUPE’ kuzinduliwa Dar, mastaa kibao ndani! first appeared on SpotiLEO.


