DAR ES SALAAM :MCHEZAJI wa kimataifa wa Burkina Faso, Stéphane Aziz Ki, ameendelea kuonesha mapenzi ya dhati kwa mke wake, Hamisa Mobetto, baada ya kumzawadia gari la kifahari aina ya G-Wagon ikiwa ni sehemu ya kusherehekea mwaka mmoja tangu wafunge ndoa.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, nyota huyo aliambatanisha video ya tukio hilo la kimapenzi lililowagusa wengi, sambamba na ujumbe mzito uliojaa shukrani, mapenzi na dua kwa mwenzi wake wa maisha.
Katika ujumbe huo, Aziz Ki aliandika:“Leo ni mwaka mmoja tangu tufunge ndoa. Asante Mungu.
“Ninashukuru kwa amani, ukuaji na maombi tunayoshirikiana.
Hiki ni kitendo kidogo tu cha kusema asante kwa kuwa mwanamke ulivyo: mvumilivu, mwenye nguvu, mwenye upendo na aliyejaa nuru.

“Hakuna zawadi wala zawadi ya gharama kubwa itakayoweza kueleza jinsi ninavyokupenda, kukuthamini na kukuabudu, mke wangu mrembo. Wewe ni baraka kwa njia nyingi.
“Mungu aendelee kutuongoza, kulinda nyumba yetu na kutuongezea upendo na maelewano, sasa na milele. Nakupenda sana.”ameandika
Ujumbe huo umeibua hisia kali mtandaoni, huku mashabiki wengi wakimpongeza kwa kuenzi ndoa yake hadharani na kuonesha mfano wa mapenzi, heshima na shukrani kwa mwenzi wake.
Zawadi hiyo ya gari la kifahari aina ya G-Wagon imezidi kudhihirisha namna mchezaji huyo anavyomthamini Hamisa, na imekuwa gumzo mitandaoni kama ishara ya mapenzi yaliyojengwa juu ya mshikamano, maombi na kuthaminiana.
Kwa wengi, tukio hilo limekuwa kumbusho kuwa mapenzi ya kweli huambatana na vitendo, si maneno pekee.
The post Aziz Ki amzawadia Hamisa G-Wagon first appeared on SpotiLEO.




