DAR ES SALAAM: MSANII maarufu wa Bongo Fleva nchini, Diamond Platnumz, ametuma ujumbe maalum kwa wanandoa na wale ambao bado hawajabahatika kuingia kwenye ndoa, akihamasisha upendo na amani kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, staa huyo alichapisha ujumbe mzito wenye maombi na dua kwa Waislamu na jamii kwa ujumla, akisisitiza umuhimu wa ndoa yenye utulivu na furaha.
“Kuelekea Mwezi Mtukufu wa Ramadhan InshaAllah Mwenyezi Mungu awafanyie wepesi kwa kila ambaye hajabahatika kuwa na ndoa aweze kupata ndoa ili kuufaidi vyema mwezi huu mtukufu wa Ramadhani,” ameandika Diamond.
Msanii huyo aliendelea kuombea ndoa zenye kudumu na zilizojaa maelewano.
“Lakini pia ndoa itakayodumu, itakayokuwa na amani, kutulizana, upendo, maendeleo na furaha tele… Tuseme Aamiin,” aliongeza.
Ujumbe huo umepokelewa kwa hisia tofauti na mashabiki wake, wengi wakimuunga mkono kwa kuhamasisha maadili ya ndoa na mshikamano wa kifamilia katika kipindi hiki cha maandalizi ya mwezi wa ibada.
Diamond Platnumz amekuwa akitumia majukwaa yake ya mitandao ya kijamii mara kwa mara kuwasilisha ujumbe wa kijamii, kidini na kuhamasisha umoja miongoni mwa wafuasi wake.
The post Diamond Platnumz awaombea wasio na ndoa first appeared on SpotiLEO.


