DAR ES SALAAM: MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Nandy, ameweka wazi kuwa mume wake, Billnass, amemuomba mwaka huu amzalie mtoto mwingine, akieleza kuwa ni wakati muafaka kwani binti yao, Naya, anakaribia kutimiza miaka minne.
Akizungumza kwa furaha, Nandy amesema mume wake anaona ni muda sahihi wa kuongeza mtoto katika familia yao.
“Mume wangu anataka nimzalie mtoto mwingine, yes bila shaka. Naya anaenda miaka minne, anaona kama nachelewa,” amesema Nandy.
Mbali na hilo, hitmaker huyo pia ameweka wazi kuhusu gari aina ya G-Wagon aliyoionesha siku ya Valentine, akifafanua kuwa alinunuliwa na Billnass kama zawadi maalum ya mapenzi.

Nandy alimshukuru mume wake kwa kugharamia gari hilo la kifahari, akieleza kuwa ni moja ya magari aliyokuwa akiota kumiliki maishani mwake.
Kauli hiyo imezua mjadala mtandaoni, huku mashabiki wengi wakipongeza mapenzi yao na namna wanavyoendelea kupeana sapoti katika ndoa yao, sambamba na kulea familia yao kwa mshikamano.
Kwa sasa, macho ya wengi yameelekezwa kwa wawili hao wakisubiri kuona kama familia yao itaongezeka hivi karibuni.
The post Nandy: Billnass ataka mtoto mwingine, first appeared on SpotiLEO.



