DAR ES SALAAM:MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Zuwena Mohammed ‘Shilole’, ameonesha furaha na upendo wake hadharani kwa kumpongeza mpenzi wake katika siku yake ya kuzaliwa, sambamba na kusherehekea miaka minne ya uhusiano wao.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Shilole alichapisha picha akiwa katika mjongeo wa kimahaba na mpenzi wake, akiambatanisha na ujumbe mzito wa upendo na shukrani uliogusa wengi wa mashabiki wake.
Katika ujumbe huo, Shilole aliweka wazi kuwa safari yao ya mapenzi imefikisha miaka minne sasa, akisisitiza kuwa Mungu amekuwa nguzo muhimu katika kila hatua ya uhusiano wao.
“Mungu akupe kuona mengi yenye heri mbele yako.
Unajua nakuombea, na nipo na wewe kwa kila hatua kwa sababu nakupenda.
Tulikotoka, tulipo, na tunapoenda… kwa miaka hii minne, Mungu ndiye ametusimamia.
Mipango yake si ya binadamu, na haijawahi kuwa rahisi, lakini bado tupo hapa kwa uweza wake.
Asante kwa kusimama na mimi, kunipa moyo na kunishika mkono kwenye nyakati zote.
Happy Birthday soulmate
Happy Birthday my love. Nakupenda.”
Mashabiki na wafuasi wake walifurika katika sehemu ya maoni wakimtakia heri mpenzi huyo pamoja na kuwapongeza kwa kudumu katika uhusiano wao kwa kipindi hicho chote.
Shilole, ambaye amekuwa akijulikana kwa uwazi wake kuhusu maisha binafsi na kazi yake ya muziki, ameendelea kuonyesha kuwa pamoja na changamoto za maisha ya umaarufu, mapenzi ya kweli yanaweza kudumu kwa imani, uvumilivu na mshikamano.
Je, huu ndio mwanzo wa hatua nyingine kubwa katika safari yao ya mapenzi? Muda ndio utakaotoa majibu.
The post Shilole aadhimisha miaka minne ya Penzi lake first appeared on SpotiLEO.


