DAR ES SALAAM:MUIGIZAJI wa filamu za Kibongo, Zaiylissa, ametangaza rasmi kufunga ndoa na mpenzi wake anayejulikana kwa jina la Mr. Said, hatua inayofungua ukurasa mpya katika maisha yake ya ndoa.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Zaiylissa ameshirikisha video fupi ikimuonyesha akiwa karibu na mume wake katika hali ya furaha na mapenzi, akiambatanisha na ujumbe mfupi lakini wenye uzito: “ALHAMDULILAH Official Mrs Said.” Ujumbe huo umeibua pongezi na maoni mbalimbali kutoka kwa mashabiki na wadau wa tasnia ya burudani.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, hii inatajwa kuwa ndoa ya nne kwa muigizaji huyo. Awali aliwahi kufunga ndoa na mzazi mwenzake, baadaye na msanii wa Bongo Fleva Dulla Makabila, kisha akafunga ndoa nyingine na Haji Manara kabla ya kuhitimisha safari hiyo.
Habari za ndoa yake mpya zimeendelea kushika kasi mitandaoni huku mashabiki wake wakimtumia salamu za heri na dua njema, wakimtakia maisha mema na yenye baraka katika ndoa yake na Mr. Said.
Kwa sasa, Zaiylissa hajatoa maelezo ya ziada kuhusu sherehe ya ndoa hiyo, lakini ujumbe wake wa “Alhamdulilah” unaashiria shukrani na matumaini mapya katika hatua hii muhimu ya maisha yake.
The post Zaiylissa afunga ndoa tena first appeared on SpotiLEO.




