KOCHA Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amesema kikosi chake kitapokea mabadiliko ya kila wakati kutokana na changamoto za ratiba nzito za mechi zinazofuata za Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Barker amesema , ili kuhakikisha kila mchezaji anapata nafasi ya kucheza na timu inabaki imara, mabadiliko ya kikosi ni lazima.
“Kulingana na ratiba ya mechi, ni lazima tufanye mabadiliko ya kikosi ili kila mchezaji apate nafasi na timu ipate matokeo mazuri,” amesema kocha huyo.
Kauli hiyo ilitolewa mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Greenland, ambapo kikosi cha Simba kilijumuisha wachezaji ambao hawakupata nafasi mara kwa mara katika mechi zilizopita.
Katika mchezo huo wa hatua ya 64 bora Simba iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Greenland, Mchezo uliopigwa Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
“Licha ya baadhi ya wachezaji kushindwa kucheza mara kwa mara, nimefurahishwa na maendeleo ya kikosi changu. Nimejipanga kukabiliana na ugumu wa ratiba, kwani ndani ya wiki moja tunaweza kucheza mechi tatu, hali inayotuhitaji kubadilisha kikosi mara kwa mara,” amesema Barker.
Kocha Barker amesisitiza kuwa mabadiliko haya hayana budi kwa lengo la kuhakikisha kila mchezaji ana mchango wake na timu inaendelea kuwa na ushindani mkubwa katika michuano yote inayoshiriki.
The post BARKER AFICHUA MBINU SIMBA KUKABILIANA NA RATIBA appeared first on Soka La Bongo.


