KLABU ya Simba SC imeingia sura mpya ya uendeshaji baada ya Katiba yake kupitishwa rasmi na Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Msajili wa Vyama vya Michezo, Abel Ngilangwa, ametangaza kuidhinishwa kwa marekebisho ya Katiba ya Simba SC, hatua inayohitimisha mchakato wa muda mrefu wa mageuzi ya uendeshaji wa klabu hiyo. Uidhinishaji huu unalenga kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji huku ukiendelea kulinda maslahi ya wanachama.
Ngilangwa amesema amekamilisha jukumu hilo kufuatia maelekezo ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, aliyemtaka kuhakikisha mchakato unahitimishwa kabla ya mwisho wa mwezi huu.
Amesisitiza kuwa hatua iliyokuwa imebaki ilikuwa ni kukabidhi Katiba iliyoidhinishwa kwa uongozi wa klabu na kusaini nyaraka za kukubaliana na marekebisho hayo, jambo ambalo limekamilika kwa mujibu wa sheria na kanuni za usajili wa vyama vya michezo.
“Simba ilianza mageuzi ya mfumo wa uendeshaji kwa lengo la kuruhusu uwekezaji kulingana na Katiba ya mwaka 2018, lakini ilikumbana na changamoto za kisheria na kiutawala, ikiwemo masuala ya umiliki, usajili wa wadhamini na uoanifu na matakwa ya taasisi za Serikali.
Marekebisho haya yalipitishwa na Mkutano Mkuu wa Wanachama Novemba 30, 2025, na kuwasilishwa kwa Msajili Desemba 10, 2025 kabla ya kurejeshwa kwa maboresho mara kadhaa hadi toleo la mwisho lililowasilishwa Februari 5, 2026,” amesema Ngilangwa.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 11 ya Kanuni za Msajili wa Vyama vya Michezo (T.S Na. 441 ya mwaka 1999), Serikali iliangalia kwa makini kisheria na kujiridhisha kuwa marekebisho haya hayaathiri usalama, amani wala maendeleo ya klabu.
Maboresho yaliyopitishwa ni pamoja na kuanzishwa kwa kampuni ya Simba Sports Club Company Limited, itakayoshughulikia shughuli za kibiashara na kiutendaji; hisa za klabu kumilikiwa kupitia Baraza la Wadhamini kwa niaba ya wanachama;
kuimarishwa kwa Baraza la Wadhamini lenye wajumbe kati ya watano hadi saba; Mkutano Mkuu kubaki chombo chenye mamlaka ya mwisho ya uteuzi na uondoaji wa wadhamini; na wanachama kubaki na angalau asilimia 51 ya hisa kulingana na sheria.
Ngilangwa ameweka wazi kuwa muundo huu hauanzishi mfumo mpya bali unatekeleza uwiano wa umiliki uliokubaliwa na wanachama.
Aidha, idhini hiyo imetolewa kwa sababu marekebisho haya yanaendana na Sheria ya BMT, yanaimarisha utawala bora na yamezingatia ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, uliotaka kuwepo kwa kampuni moja ya uendeshaji huku mali zisizohamishika zikibaki mikononi mwa wanachama kupitia wadhamini.
Mabadiliko haya yameondoa changamoto za kisheria zilizokuwa zinakwamisha mchakato, hasa kuhusu uoanifu na taasisi kama RITA na FCC, na kuweka msingi imara wa usimamizi wa mali na uwekezaji.
Ngilangwa ameongeza kuwa Serikali haina jukumu la kuamua mfumo wa uendeshaji wa klabu, bali ni kuidhinisha maboresho yanayokidhi matakwa ya sheria baada ya wanachama kufanya maamuzi yao.
Ametoa wito kwa wanachama na wadau wa Simba kuheshimu maamuzi haya ili klabu iendelee kwa utulivu, mshikamano na mafanikio zaidi.
The post SIMBA YATUMBUA SURA MPYA, WADHAMINI WASHIKILIA HISA appeared first on Soka La Bongo.



