KOCHA Mkuu wa timu ya B19 maarufu kama Mabeberu wa Jiji, Twaha Beimbaya amesema mchezo wao dhidi ya Simba SC umekuwa somo kubwa kwa kikosi chake, akieleza kuwa vijana wake wamepata uzoefu mkubwa licha ya kuondolewa katika hatua ya 32 ya Kombe la Shirikisho la CRDB.
Katika mchezo huo uliochezwa jana usiku kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar es Salaam, B19 walilazimika kuaga mashindano hayo baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 kutoka kwa Simba, matokeo yaliyothibitisha ubora wa wapinzani wao katika mechi hiyo.
Beimbaya amesema kuwa pamoja na matokeo hayo, kikosi chake kilijitahidi kupambana kadiri kilivyoweza, lakini uzoefu mkubwa wa wachezaji wa Simba uliwapa faida kubwa katika kutumia makosa yaliyojitokeza upande wa wapinzani wao.
Ameongeza kuwa bao la kwanza walilofungwa lilitokana na uzembe wa mchezaji mmoja mmoja, hali iliyowapa Simba nafasi ya kujiamini zaidi na kuendeleza presha ambayo hatimaye iliwawezesha kupata ushindi huo.
Kocha huyo amesema kabla ya mchezo aliwapa maelekezo maalum wachezaji wake ili waweze kucheza kwa nidhamu na kufuata mbinu walizopanga, na kwa kiasi kikubwa walijitahidi kuyatekeleza licha ya kukutana na upinzani mkali.
“Simba ni timu kubwa, niliwapa maelekezo vijana wangu na kwa kiasi fulani walijitahidi kuyafuata, lakini kutokana na uzoefu na ubora wa mpinzani wetu waliweza kutumia makosa yetu na kupata ushindi,” alisema Beimbaya.
Amesisitiza kuwa wanachokichukua kutoka katika mchezo huo ni uzoefu na mafunzo muhimu yatakayowasaidia katika michezo ya Championship, akiamini kuwa wakifanyia kazi makosa yao wana nafasi nzuri ya kurejea tena katika Kombe la Shirikisho la CRDB msimu ujao na kufanya vizuri zaidi.
The post BEI MBAYA AKIRI SIMBA IMEMFUNDISHA SOMO ZITO appeared first on SOKALEO.



