Na Mwandishi Wetu, Lindi
Mahakama ya Wilaya ya Nachingwea, mkoani Lindi, imemhukumu Omari Ntauka kifungo cha miaka 22 jela baada ya kupatikana na hatia ya makosa ya uhujumu uchumi na kusababisha hasara ya Shilingi 5,602,100 kwa kuiba kilogramu 1,855 za ufuta alizokabidhiwa na wakulima. Ufuta huo ulikuwa wa msimu wa mwaka 2021/2022 katika tawi la Chilonji, kupitia Chama cha Msingi cha Ushirika (AMCOS) cha Rweje.
Mahakamani ilielezwa kuwa mshtakiwa, ambaye alikuwa Karani wa AMCOS ya Rweje, alisababisha hasara hiyo kwa makusudi, akikitumia vibaya cheo chake na kukiathiri chama hicho.
Kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 21147/2024, ya Jamhuri dhidi ya Ntauka, ilisikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Mhe. Neema Mhelela, huku upande wa mashtaka ukiwakilishwa na Wakili wa Serikali Haruna Mchande kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Lindi.
Katika hukumu iliyotolewa Novemba 11, 2024, kosa la kwanza alilopatikana nalo ni kusababisha hasara kwa mamlaka kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza na kifungu cha 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi, Sura ya 200, marejeo ya mwaka 2022.
Kosa la pili ni wizi, kinyume na kifungu cha 271 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa amehukumiwa kifungo cha miaka 20 kwa kosa la kwanza na miaka miwili kwa kosa la pili, hivyo kufanya jumla ya miaka 22 jela. Aidha, ameamriwa kulipa kiasi cha Shilingi 5,602,100 ili kufidia hasara aliyosababisha kwa chama hicho cha msingi.