Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo (Mb.) akishiriki Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi za Afrika na Urusi uliofanyika tarehe 8 na 9 Novemba, 2024 jijini Sochi, Urusi. |
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. Dennis Londo amesisitiza umuhimu wa nguvu ya pamoja katika kumaliza changamoto za kidunia na kuleta ustawi katika jamii ili kuyafikia maendeleo endelevu.
Msisitizo huo ameutoa alipokuwa akitoa salamu za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mahmoud Thabit Kombo katika Mkutano wa Kwanza wa Mawaziri wa Mambo ya Nje kutoka nchi za Afrika na Shirikisho la Urusi uliofanyika tarehe 9 hadi 10 Novemba, 2024 mjini Sochi, Urusi na kuongozwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Shirikisho la Urusi, Mhe. Bogdanov Mikhail Leonidovich.
Pamoja na salamu hizo Mhe. Londo ameeleza kuwa Nchi za Afrika na Urusi zimekuwa na historia nzuri tangu enzi za harakati za ukombozi wa bara hilo ambapo nchi ya Urusi ilisaidia nchi mbalimbali barani Afika ili kupata Uhuru. Aidha, Ushirikiano huo umendelea kwa kushirikiana katika kutatua changamoto mbalimbali za kidunia ikiwemo kukosekana kwa amani, usawa na kutojitosheleza, kadhalika kushirikiana kutatua migogoro ya kiuharifu, ugaidi na vita vinavyopelekea kupoteza maisha ya watu wake wasio na hatia.
Vilevile, Mhe. Londo ameleza kuwa njaa, magonjwa ya kuambukiza na umasikini vimekuwa vihatarishi vya usalama kwa nchi hizo na hivyo ili kupata suluhisho la changamoto hizo unahitajika ushirikiano imara kutoka pande zote utakaoenda sambamba na maono ya pamoja ya kiongozi na kiutawala.
‘’ Mkutano huu unaweza kuweka mikakati ya utatuzi wa changamoto tunazopitia na kuidhihirishia dunia kuwa ushirikiano imara unaweza kumaliza changamoto za pamoja ambazo zimekuwa kikwazo katika kufikia malengo ya maendeleo endelevu kwa ustawi wa maisha ya watu wetu na Taifa kwa ujumla’’, alisisitiza Mhe. Londo.
Pia, alieleza kuwa kufanikiwa kwa jitihada hizo za umoja na mshikamano kutapelekea kuelekeza nguvu ya pamoja katika maeneo ya kimkakati ya ushirikiano ikiwemo uwekezaji katika usalama wa chakula, biashara, ushirikiano wa kiuchumi, kushirikiana kumaliza ugaidi, kuimarisha sekta ya afya, ulinzi, na kujenga uwezo katika masuala ya kidijitali na teknolojia.
Pamoja na masuala mengine, Mhe. Londo ameeleza nia ya dhati ya Tanzania ya kushirikiana na Urusi na Afrika katika kukuza biashara na uwekezaji na kwamba katika miaka mitano iliyopita ushirikiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Urusi umekua kutoka dola za kimarekani 54,243,713 mwaka 2019 hadi dola za kimarekani 390,388,000 mwaka 2023.
Aidha, ameeleza kuwa kuwepo kwa utaratibu wa pamoja wa Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) umekuwa kichocheo cha kukuza biashara barani Afrika kwa kuondoa tozo, kukuza viwanda, kukuza biashara na uwekezaji ndani ya Afrika na kuleta ajira miongoni mwa vijana ambao ndio nguvu kazi ya nchi hizo.
Urusi imekuwa ikisafirisha bidhaa zake barani Afrika mara 5 zaidi ya Afrika, na kwamba hii ni moja ya changamoto inayopelekea kushuka kwa maendeleo ya biashara na kiuchumi. Akasisitiza kuwa Urusi inaweza kuwekeza Afrika kupitia kampuni zake za biashara na uwekezaji ambazo zitasaidia kukuza viwanda vya uzalishaji vya Afrika, kuijengea Afrika uwezo katika masuala ya kiufundi na kuanzisha taasisi imara na zenye nguvu kibiashara.
Hata hivyo, inakadiriwa dola za kimarekani Trillion 3 katika soko huru la Afrika zinaweza kumaliza umasikini, kuleta usawa na kukuza uchumi na kuiweka Afrika katika ukuaji jumuishi na endelevu.
Pia aliishukuru Serikali ya Urusi kwa kauli yake ya kuendelea kuisaidia Afrika katika suala la kujenga uwezo kwenye biashara na teknolojia hususan katika sekta za uzalishaji ambazo zitaiwezesha Afrika kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazokidhi vigezo vya kimataifa.