NA WILLIUM PAUL, Moshi.
MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Moshi mkoa wa Kilimanjaro wameomba serikali kutoa kwa wakati fedha za bajeti zilizopangwa ili kurahisisha utekelezaji wa shughulii za maendeleo kama iliyokusudiwa.
Wakizungumza katika baraza la madiwani la kupitia taarifa ya hesabu za mwisho za Halmashauri ya wilaya Moshi kwa mwaka wa fedha ulioisha June 30/2024 madiwani wa Halmashauri ya Moshi baadhi ya madiwani hao akiwemo Kamili Mmbando diwani kata ya Kahe Mashariki.
Wamesema ili kukabiliana na mapungufu na hoja za mkaguzi wa hesabu za serikali CAG ni vyema serikali kuweka fedha kwa wakati kutokana na kuwepo kwa fedha zinazowekwa ukiwa umebaki muda mchache wa kufunga mwaka wa serikali.
Alex Umbela ni diwani wa kata ya Kirua Vunjo Mashariki amesema ili kuondokana na tatizo la kuvuka na fedha nyingi kwenda mwaka mwingine, ameshauri Halmashauri kuongeza kasi zaidi ili kuondoa dhana ya serikali kupunguza bajeti katika mwaka ujao kutokana na kuonekana Halmashauri kushindwa kuzitumia.
Naye Wilhad Kitali diwani wa kata ya Uru Mashariki, amesema ili kuendana na kaulimbiu ya serikali ya awamu ya sita chini ya raisi dk Samia Suluhu Hassan, ya kazi iendelee ” ni lazima jitihada za makusudi zichukuliwe kufanikisha maendeleo kwa wananchi.
Akikiri kujitokeza kwa changamoto hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Moshi Shadrack Mhagama, amesema kuchelewesha kuwekwa fedha za matumizi ya miradi na kawaida Hali ambayo inasababisha kushindwa kuzitumia kama inavyopaswa.
“Ni kweli Halmashauri tukipokea fedha zaidi ya bilioni 4 mwishoni mwa mwezi wa sita za kutekeleza miradi ya maendeleo ya elimu ikiwemo ujenzi wa shule mpya za sekondari zikiwemo za amali na jiji ngazi ya kata na shule moja ya msingi ambapo kwa kipindi cha muda huo mfupi isingewezekana utekelezaji wake”
Aliongeza kuwa endapo fedha hiyo ingetoka kwa wakati muhafaka utekelezaji wake kwenye miradi hiyo ya maendeleo ungefanyika kwa ufanisi sambamba na miradi iliyokwisha kufanyika kwa fedha zilizotolewa ndani ya muda.
Baraza hilo Maalumu la kupitia taarifa ya hesabu za mwisho za Halmashauri ya wilaya ya Moshi kwa mwaka wa fedha ulioisha June 30 2024 limehidhuriwa na viongozi wa serikali akiwemo kaimu Katibu tawala mkoa wa Kilimanjaro.