Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA), imewataka wauzaji wakubwa wa kemikali kuacha kuwauzia wauzaji wa kati na wadogo wa kemikali ambao hawajasajiliwa kufanya biashara hiyo.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo, wakati wa kikao na wadau wanaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa kemikali bashirifu kilichoandaliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na kufanyika katika Ofisi za Kanda ya Mashariki jijini Dar es Salaam.
“Wadau wote wa kemikali lazima wawe wamesajiliwa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa mujibu wa sheria pamoja na kutimiza maazimio tulioweka ili waweze kufanya biashara zao kwa usalama ili kulinda afya za binadamu na mazingira,” alisema Mkurugenzi Ndiyo.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Sayansi Jinai kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Ziliwa Machibya, amesema kuwa kemikali bashirifu ni hatari katika mazingira ya matumizi ya dawa za kulevya hivyo, amewasihi wadau wa kemikali bashirifu kufuata taratibu za usajili ili ziweze kutumika katika matumizi yaliyokusudiwa katika uzalishaji mbalimbali na kwa usalama.
Kwa upande wake Geoffrey Jato ambaye ni mdau wa kemikali ameipongeza Mamlaka kwa kuwapa elimu na kuendelea kuweka ushirikiano wa karibu na wadau wa kemikali jambo ambalo limeweza kuwatatulia changamoto mbalimbali zikiwemo usajili.
“Elimu tuliyoipata ya usajili wadau wengi hawakua nayo, ila kwa sasa wingi utaongezeka wa wadau kujisajili na kupata elimu ili wanapofanya manunuzi ya kemikali au uzalishaji waweze kufanya kwa usalama,” alisema Jato.
Mkurugenzi wa Huduma za Udhibiti, Daniel Ndiyo (katikati) akiwa na Viongozi pamoja na Wadau wa Kemikali Bashirifu mara baada ya kikao na wadau hao kilichofanyika jijini Dar es Salaam Novemba 13, 2024.