Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Bingwa was mashindano ya Samia Supa Cup ya Kata ya Msasani atazawadiwa fedha taslimu, Sh4 million, Diwani wa Kata hiyo, Luca Neghest ametangaza.
Neghest alisema hayo wakati wa uzinduzi rasmi uliofanyika kwenye ufukwe wa Coco (Coco Beach) na kushirikisha mamia ya wadau wa michezo ambao, pia walishiriki katika matembezi maalum kwa ajili ya ufunguzi wa mashindano hayo.
Uzinduzi huo pia ulipambwa na michezo mbalimbali pamoja na burudani kutoka bendi namba moja nchini, African Stars wana Twanga Pepeta.
Neghest alisema kuwa zawadi hiyo itakuwa kwa mashindano ya soka na mchezo wa rede kwa wanawake ambapo washindi wa pili watazawadiwa Sh 2 milioni kila mmoja.
Alisema kuwa mshindi wa kwanza kwa mchezo wa drafti atazawadiwa sh 2 milioni wakati mshindi wa pili atazawadiwa Sh milioni moja.
Kwa upande wa bao, Neghesti alisema kuwa mshindi atapata Sh 1 milioni na mshindi wa pili atazawadisha Sh500, 000.
Alisema kuwa maandalizi ya mashindano hayo yaliyopangwa kuanza Desemba 9, 2024 yanaendelea vizuri na yanatarajiwa kuwa na ushindi na msisimko mkubwa.
“Kila mwaka, Kata ya Msasani imekuwa nikiandaa mashindano ya Diwani Cup, safari hii tumebadilika na kuandaa mashindano ya Samia Supa Cup kwa lengo la kutambua uongozi wake bora nchini, situ katika sekta ya michezo, bali katika sekta mbalimbali.Tumeomba ruhusa kutumia jina lake na tumekubaliwa. Pia lengo liingine la kuandaa mashindano haya ni kuhamasisha Watanzania kujitokeza katika zoezi la kupiga kura na kuchagua viongozi bora wa serikali ya mtaa na wala siyo kumchagua bora kiongozi,”alisema Neghest.
Alifafanua kuwa timu mbalimbali katika kata ya Msasani kwa sasa zipo katika maandalizi makali kwa ajili ya mashindano hayo na karibu timu zote zimepania kutwaa ubingwa.
“Kila Mtanzania anafahamu jinsi Rais, Mama Samia Suluhu Hassan amechangia maendeleo ya michezo na katika sekta nyingine. Anastahili kupewa shukrani na pongezi kwa kazi nzuri ya kuitangaza Tanzania nje ya mikapa yake na kuleta maendeleo,” alisema Neghest.