Na Mwandishi wetu ,Arusha.
Wajumbe na wanachama wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) zaidi ya 800,wametembelea mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania dkt.Samia Suluhu Hassan katika sekta ya Utalii.
Ziara hiyo iliyopewa Jina la TUGHE ROYAL TOUR inafanyika mara baada ya kumaliza kwa kikao kazi cha siku tano Jijini Arusha,kilichowashirikisha Waajiri na Viongozi wa Matawi nchini.
Akizungumza na Vyombo vya habari katika ziara hiyo Mwenyekiti wa TUGHE Taifa Bw. Joel George Kaminyoge alisema lengo la ziara hiyo ni kutoa hamasa ya utalii wa ndani na kuunga mkono jitihada za Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kukuza utalii ambapo ziara hiyo imewapa fursa wanachama wao kujionea vivutio vya kipekee vinavyopatikana hifadhi ya Ngorongoro.
“Leo tumekuja na wanachama zaidi ya 800 kutembelea Kreta ya Ngorongoro kujionea moja kati ya vivutio lakini pia kuhamasisha watanzania kuendelea kutembelea hifadhi zetu ili kuweza kujionea vivutio hivi na kukuza utalii wa ndani”Alisisitiza Kaminyoge
Aidha alisema kuwa kuwa anaamini ziara hiyo italeta tija na hamasa kwa wakuu wa taasisi kuwa na utaratibu wa kuwapeleka watumishi wao kufanya utalii wa ndani katika vivutio mbalimbali nchini.
Nae Katibu Mkuu wa TUGHE Taifa bw.Hery Mkunda alisema kuwa wameamua kufanya kwa vitendo kwa kufanya Utalii wa ndani,na kujifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na afya ya akili ambayo itawasaidia kuwa imara kiakili,kuwa na morali warejeapo makazini.
“Ziara hii imeshirikisha magari zaidi ya 110 na watalii zaidi ya 800,na hii yote ni kumuunga mkono mheshimiwa Raisi Samia na kuhamsisha utalii wa ndani na sisi tumeita TUGHE ROYAL TOUR 2024,Tuendelee kutembelea hifadhi kdiri inavyowezekana.”Alisema bw.Mkunda
Akiwapokea wageni Meneja wa huduma za Utalii na masoko wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro Bi.Mariam Kobelo, alisema kwamba Mamlaka hiyo ipo tayari kuendelea kupokea makundi mbalimbali ya wageni na kuwahakikishia kuwa wanapata huduma bora ili kuendelea kutangaza hifadhi hiyo na kuimarisha utalii ndani.
Hata hivyo alitoa rai kwa watanzania kuhakikisha kuwa wanaendelea kutembelea hifadhi zilizopo nchini kwa kuwa huduma nyingi zimepunguzwa na pia kutengenezwa kwa mazingira wezeshi ya kila mtanzania kumudu gharama za kuingia na kufika hifadhini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Tanzanite Cooperates L.t.d waratibu wa ziara hiyo Bi. Elina Mwangomo, alieleza kuwa kwa sasa kuna ongezeko kubwa la watalii wa ndani hali inayoongeza hamasa kwa wadau wa utalii kuendelea kuboresha, huduma zao.
“Tunqmshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuwekea mazingira wezeshi kwani baada ya filamu ya Royal Tour kumekuwa na mwamko mkubwa wa utalii ambao umetusaidia sisi wadau wa Utalii kupata fursa ya kupokea watalii wengi zaidi, mfano leo tumeweza kuingia Ngorongoro na watalii wa ndani zaidi ya 800 na naamini makundi haya yataendelea kuja kwa wingi” Aliesema Bi. Elina Mwangomo.
Mmoja wa wanachama wa TUGHE bi.Jackline Ngoda ambaye ni mmoja kati ya wanachama waliotembelea Hifadhi hiyo ameonesha kufurahishwa na ziara hiyo baada ya kujionea Wanyama mbalimbali ikiwepo wanyama wakubwa watano (Big 5) wakiwa katika maeneo yao ya asili.
Ziara hii ni sehemu ya Juhudi za TUGHE kuwaleta pamoja waajiri na wafanyakazi wa taasisi za Serikali kupata nafasi ya kujifunza na kujenga uhusiano na ushirikiano nje ya mazingira rasmi ya kazi.
Ngorongoro imekuwa moja kati ya eneo ambalo linapendwa zaidi na wageni na watalii kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kutokana na maajabu yaliyomo ikiwemo Wanyama wakubwa watano(Big 5) na Kreta.