Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umetangaza hatua kubwa katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kupitia mifumo ya kidijitali, kufuatia utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha mifumo ya taasisi za serikali inasomana.
Akizungumza leo jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Irene Kisaka, amesema mifumo hiyo imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya afya kwa kuondoa usumbufu wa wananchi kutembea na taarifa zao wanapohitaji huduma za afya. “Sasa mgonjwa anaweza kupatiwa huduma popote, hata bila kitambulisho cha bima, kwani taarifa zake zinapatikana moja kwa moja kwenye mfumo,” amesema Kisaka.
Mifumo hii ya kidijitali pia imepunguza kwa kiasi kikubwa udanganyifu katika madai ya matibabu na fedha, huku ikiharakisha mchakato wa huduma kwa wagonjwa.
Pamoja na maboresho haya, NHIF imetoa wito kwa vyombo vya habari kushirikiana katika kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza, ambayo yamekuwa yakisababisha gharama kubwa za matibabu.
Hatua hizi ni sehemu ya jitihada za NHIF kuhakikisha huduma za afya zinapatikana kwa urahisi na kwa ufanisi, huku ikiwalenga wananchi wote kufurahia bima ya afya bora na endelevu.