Mkurugenzi mkuu ZAFELA Jamila Mahmoud Juma akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa Mpango Mkakati Jumuishi wa Jinsia katika Michezo hafla iliofanyika katika Uwanja wa Mpira wa Mao Zedong Mpirani Zanzibar.








Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Riziki Pembe Juma amesema uimarishwaji wa ulinzi na usalama katika Sekta ya michezo itasaidia kuboresaha mazingira bora ya michezo kwa washiriki na kuzingatia usawa wa kijinsia.
Akizungumza katika Uzinduzi wa Mpango Mkakati Jumuishi wa Jinsia katika Michezo Zanzibar ulifanyika katika Uwanja wa Mao Zedong Mpirani amesema michezo ni jukwaa salama, jumuishi na lenye usawa wa kijinsia kwa kila mshiriki.
Amesema hiyo ni hatua ya kimkakati inayolenga kuimarisha usawa wa kijinsia katika michezo ili kufanikisha kauli mbiu ya sera ya michezo ya mwaka 2018 ambayo inasema “MICHEZO KWA WOTE”
“Kauli hii humaanisha kuwa kila mmoja awepo katika michezo bila ya kujali jinsi hata hali ya mtu kwani hata wenye mahitaji maalum wanapaswa kushiriki” alieleza Waziri Pembe.
Amefahamisha kuwa kupitia mpango huo utasaidia kuweka dira na hatua madhubuti itakayofanikisha maendeleo katika sekta ya michezo kuwa jumuishi na kuzingatia usawa wa kijinsia na kuleta mabadiliko chanya.
Aidha amesema mpango huo ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha wanawake na wanaume wanapata fursa sawa za kushiriki na kuongoza ili kufanikisha maendeleo katika sekta ya michezo pamoja na kuwawesha wanawake kushiriki kikamilifu katika michezo kuanzia ngazi ya jamii hadi taifa.
“Kumekuwa na changamoto nyingi kwa wanawake kushiriki michezo hivyo muuongoza huu umekuja kuondoa changamoto na vizuizi vya kitamaduni na miundombinu ambayo tuzuia wanawake” alisema waziri huyo.
Amebaiinisha kuwa kupitia mpango huo utasaidia kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha usambazaji wa rasilimali katika sekta ya michezo unazingatia mahitaji na fursa sawa kwa wote bila ya ubaguzi wa kijinsia sambamba na kutoa fursa za mafunzo ya uongozi katika sekta ya michezo kwa jinsia zote.
Amesisitiza kuwa kutofumbua macho vitendo vya udhalilishaji pamoja na kuachana na muhali ili kuendelea kuvitokomeza vitendo hivyo katika jamii yetu kwani katika sekta ya michezo vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, hisia na kimwili vimekuwa vikijitokeza mara nyingi.
Akitoa wito kwa viongozi na wadau wa michezo kushirikiana kwa pamoja ili kufanikisha malengo ya michezo salama, jumuishi na yenye usawa wa kijinsia yanazingatiwa ili yaliyokusudiwa yawafikie wananchi kwa urahisi na kuleta maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Afisa Mdhamini wa Wizara hiyo Mfamau Lali Mfamau amesema lengo la Wizara kufanikisha dhamira moja ya kuendeleza usawa wa kijinsia, jumuishi na uwezo wa michezo katika kuleta mabadiliko.
Kwa upande wake Meneja wa kanda ya Michezo kwa Maendeleo Barani Afrika (GIZ) Kristin Richter amesema watahakikisha wanakuza usawa wa kijinsia na ujumuisha kupitia michezo kwa kuhakikisha upatikanaji wa fursa sawa kwa wanawake, wasichana na watu wenye mahitaji maalum.
Uzinduzi wa mpango mkakati huo umefanikiwa kwa ushirkiano wa Shirika la MAendeleo ya Ujerumani kupitia GIZ na Mradi wa Michezo kwa Maendeleo ya Afrika, pamoja na mashirika ya kijamii kama vile Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA), Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar pamoja na vyama vya Michezo.