Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi SACP Kaster Ngonyani akizumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo.
……
Na. Zillipa Joseph, Katavi.
Jeshi la polisi mkoani Katavi limefanikiwa kuwakamata watuhimwa 56 kwa makosa mbalimbali katika kipindi cha mwezi mmoja wa Novemba.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari mapema leo Kamanda wa Polisi mkoa wa Katavi SACP Kaster Ngonyani alisema kati ya watuhumiwa hao 17 wamekamatwa na vitu vinavyodhaniwa ni vya wizi zikiwemo pikipiki mbili, waya za uzio za kampuni ya TTCL, machine ya kuchomea vyuma, nondo 121 na machine moja ya kusaga nafaka.
Vitu vingine ni pamoja na redio ya sabufa moja na twita zake, mifuko minne ya mbolea na bando sita za mifuko ya sandalusi.
Kamanda Ngonyani alieleza kuwa watuhumiwa wanne walikamatwa na nyama pori kilogramu 15 inayodhaniwa kuwa ni ya mnyama nyati.
Aliongeza kuwa watuhumiwa kumi na moja walikutwa na kete 159 za bangi na watuhumiwa 24 walikutwa na pombe aina ya Moshi kiasi cha lita 124.
Akizungumzia mafanikio ya jeshi la polisi katika kesi walizopeleka mahakamani alisema watuhumiwa 21 walipatikana na hatia ya makosa mbalimbali ikiwemo kubaka, kuchoma nyumba, wizi, kukutwa na bangi na kujeruhi na wamehukumiwa kulingana na makosa yao.
Kamanda Ngonyani ameendelea kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na jeshi la polisi hasa katika utoaji wa ushahidi mahakamani ili kesi ziweze kupata mafanikio.