Na Farida Ramadhani na Chedaiwe Msuya, WF – Dar es Salaam.
Serikali
imesema itaendelea kuchukua hatua kali kwa taasisi zote zininazotoa
huduma za fedha kinyume cha sheria kwa kutoa mikopo umiza (kausha damu)
na kuwakandamiza wananchi.
Onyo hilo limetolewa jijini Dar es
Salaam na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba Madelu (Mb),
wakati akizindua Jukwaa la kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka
2024.
Dkt. Nchemba alisema taasisi hizo zimekuwa zikiwaumiza
wananchi kwa kutoa mikopo yenye riba kubwa pamoja na kupanga njama za
kuwafilisi wale ambao wanajua wazi hawatoweza kulipa mikopo hiyo.
Aliwataka
wadau wa Sekta ya Fedha hususan benki kuendelea kutoa elimu ya umuhimu
wa kutumia huduma rasmi za fedha kwa kutumia taasisi ambazo zimesajiliwa
ili kuepukana na madhara wanayokumbana nayo katika taasisi nyonyaji
zinazotoa mikopo umiza (kausha damu).
“Lazima wananchi wajue
kutoafautisha kati ya Taasisi rasmi na hizo zisizo rasmi, lazima
tuwaoneshe wananchi kuwa hawako salama wanapokopa kwenye taasisi zisizo
rasmi na kuwahamasisha kuwa benki ni salama zaidi”, alibainisha Dkt.
Nchemba.
Alisema ni vema wadau wa Sekta ya Fedha wawaelimishe
wananchi kuhusu umuhimu wa kutumia benki kupata mikopo pamoja na kutunza
fedha zao kwa kuwa kutunza fedha benki ni utaratibu wa kisasa wa
uendeshaji wa uchumi.
” Bado kuna baadhi ya maeneo wananchi
wanaogopa kuweka fedha benki, kwa kuwa nyinyi mpo kwenye Sekta hii
mshirikiane na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwaeleza wananchi kuwa
wasiogope kuweka fedha benki ”, alifafanua Dkt. Nchemba.
Alisema
pamoja na kazi nzuri iliyofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya
kukusanya kodi kwa weledi na kwa kufuata sheria bado wananchi
hawajaeleweshwa vizuri kuhusu kuweka fedha benki.
Aliwaagiza
viongozi wa Taasisi za Fedha nchini kujiridhisha kabla ya kuruhusu
watumishi na madalali wao kupiga minada ya mali za wadaiwa mikopo kwenye
Taasisi zao kwa kuwa kuna taarifa kuwa baadhi ya watumishi wasio
waaminifu hushirikiana na watu wengine kuwadhulumu mali zilizowekwa
kwama dhamana na kuwatia watu umasikini.
”Kuna baadhi ya maeneo
hakufanyiki vizuri katika kudai mikopo, mteja amelipa mkopo wake kwa
asilimia 80, amebakiza asilimia 20, anatokea mteja mwingine anapenda
dhamana ya mkopo iliyowekwa, benki inaamua kupiga mnada wa muda mfupi
ambao wanajua mteja hatoweza kulipa ili wamfilisi, mtu amelipa mkopo kwa
asilimia 80 halafu unauza dhamana yake ili kufidia asilimia 20 ambayo
hajalipia huko ni kumtia umaskini, huu sio utaratibu mzuri wa kujenga
sekta ya fedha na sio utaratibu mzuri wa kujenga ustawi wa jamii”,
aliongeza Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba aliziagiza Benki
kuwachukulia hatua kali baadhi ya watumishi wa benki wasio waaminifu
ambao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya wateja kuongeza mikopo
chechefu.
Aidha, aliwaagiza wadua wa Sekta ya Fedha kuendelea
kuwasisitiza wananchi kuwa fedha za mkopo zitumike kwenye shughuli za
uzalishaji kwa sababu shughuli zinazoweza kuzalisha ndio zinazoweza
kurejesha mkopo huku akitolea mfano nchi inapokopa fedha zinapelekwa
kwenye miradi mahusi ya maendeleo, kwasababu miradi ya maendeleo ndio
inaweza kuzalisha na kulipa deni na haijawahi kukopa kwa ajili ya
kulipa mishahara.
Alisema kutokana na kupeleka fedha kwenye
miradi ya maendeleo ndio maana Tanzania ni miongoni mwa nchi mbili pekee
barani Afrika zenye uhimilivu wa deni na kwa Afrika Mashariki na nchi
zilizopo katika Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Tanzania
inaongooza.
Kwa upande wake Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda alisema mwakani Serikali itaanzisha
Mtaala Mpya wa masomo ambapo somo la masuala ya fedha na ujasiriamali
litakuwa ni la lazima ili kuwaezesha wanafunzi watakapo maliza masomo
yao kuweza kujiajiri.
Aliwataka wadau mbalimbali kuendelea kutoa maoni kuhusu mtaala huo ili kuuwezesha kufikia lengo kusudiwa.
Naye
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba alisema Wizara
ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa Sekta ya Fedha nchini imeandaa
Jukwaa la wadau wa Sekta ya Fedha ili kubadilishana mawazo na uzoefu,
kupeana taarifa, kujengeana uwezo, kushirikishana katika mafanikio na
changamoto na kutafuta suluhu ya pamoja kwa changamoto zinazoikabili
sekta ya fedha nchini.
Alisema malengo ya Jukwaa la Wadau wa
Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024 ni pamoja na kutoa taarifa kuhusu
utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha kwa kipindi
cha miaka mitatu (2020/21-2023/24) na kushirikishana mbinu bora za
kiutendaji na uzoefu katika Sekta ya Fedha.
Dkt. Mwamba alisema
malengo mengine ni kujadili fursa na hatua mbalimbali zilizochukuliwa
katika kuboresha sekta ya Fedha pamoja na kushirikishana namna bora ya
kukuza matumizi ya teknolojia na uvumbuzi ili kukuza na kuimarisha Sekta
ya Fedha.
Aliongeza
kuwa Jukwaa hilo pia linalenga kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wadau
wa Sekta ya Fedha na kuufahamisha Umma juu ya hatua za maboresho
mbalimbali ya kisera na kisheria yaliyofanyika ili kuimarisha Sekta ya
Fedha nchini.
Waziri
wa Fedha, Mhe, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (Katikati), akizindua
moja ya nyaraka zilizoandaliwa za Sekta ya Fedha ambazo ni Mkakati wa
Upatikanaji wa Fedha kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Mwaka
2023/24 – 2028/29, Mwongozo wa Mitaji Halaiki (Crowd financing) pamoja
na Mwongozo wa Utoaji Hati Fungani zinazozingatia Sharia kwa Kampuni na
Taasisi za Umma wa Mwaka 2023 (Capital Markets and Securities (Corporate
and Subnational SUKUK Bonds) Guidelines-2023, wakati wa hafla ya
uzinduzi wa Jukwaa la Kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024,
katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Fedha, Mhe, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizingumza wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa
mwaka 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es
Salaam, ambazo ni Mkakati wa Upatikanaji wa Fedha kwa Wajasiriamali
Wadogo na wa Kati wa Mwaka 2023/24 – 2028/29, Mwongozo wa Mitaji Halaiki
(Crowd financing) pamoja na Mwongozo wa Utoaji Hati Fungani
zinazozingatia Sharia kwa Kampuni na Taasisi za Umma wa Mwaka 2023
(Capital Markets and Securities (Corporate and Subnational SUKUK Bonds)
Guidelines-2023, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Kwanza la
Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa
Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Fedha, Mhe, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda (wa tatu kushoto), Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba (watatu kulia), Naibu
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bi. Sauda Msemo (wapili kushoto)
wakiwa pamoja na viongozi wengine wa Serikali, wakionesha nyaraka
zilizoandaliwa za Sekta ya Fedha ambazo ni Mkakati wa Upatikanaji wa
Fedha kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Mwaka 2023/24 – 2028/29,
Mwongozo wa Mitaji Halaiki (Crowd financing) pamoja na Mwongozo wa
Utoaji Hati Fungani zinazozingatia Sharia kwa Kampuni na Taasisi za Umma
wa Mwaka 2023 (Capital Markets and Securities (Corporate and
Subnational SUKUK Bonds) Guidelines-2023, wakati wa hafla ya uzinduzi wa
Jukwaa la Kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024, katika
Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam
Wadau
mbalimbali wa Sekta ya Fedha, wakifuatilia hotuba ya Ufunguzi ya Waziri
wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani),
wakati akizundua Jukwaa la Kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka
2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam,
ambapo alitumia fursa hiyo ambazo ni Mkakati wa Upatikanaji wa Fedha kwa
Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Mwaka 2023/24 – 2028/29, Mwongozo wa
Mitaji Halaiki (Crowd financing) pamoja na Mwongozo wa Utoaji Hati
Fungani zinazozingatia Sharia kwa Kampuni na Taasisi za Umma wa Mwaka
2023 (Capital Markets and Securities (Corporate and Subnational SUKUK
Bonds) Guidelines-2023, wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Kwanza
la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa mwaka 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa
Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
Waziri
wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof. Adolf Mkenda, akizungumza
jambo wakati wa hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Kwanza la Wadau wa Sekta
ya Fedha kwa mwaka 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City,
jijini Dar es Salaam, ambapo aliipongeza Wizara ya Fedha kwa kuandaa
Jukwaa hilo na kwamba Wizara yake imetambua umuhimu wa masuala ya uchumi
na fedha na imeandaa Mtaala Mpya wa Elimu utakao wawezesha wanafunzi
kupata elimu ya ujasiriamali pamoja na biashara ili kuwajengea maarifa
ya kujiajiri na kujikwamua kiuchumi.
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, akizungumza wakati wa
hafla ya uzinduzi wa Jukwaa la Kwanza la Wadau wa Sekta ya Fedha kwa
mwaka 2024, katika Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar es
Salaam, ambapo alisema kuwa Wizara ya Fedha kwa kushirikiana na wadau wa
Sekta ya Fedha nchini imeandaa Jukwaa hilo ili kubadilishana mawazo na
uzoefu, kupeana taarifa, kujengeana uwezo, kushirikishana katika
mafanikio na changamoto na kutafuta suluhu ya pamoja kwa changamoto
zinazoikabili sekta ya fedha nchini.
(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dar es Salaam)