Baadhi ya Wananchi wa jamii ya Wafugaji wa kitonngoji cha Chilundundu kata ya Misechela wakisubiri kupata huduma ya uchunguzi na matibabu ya Ugonjwa wa kifua kikuu kutoka Wataalam wa kitengo cha kifua Kikuu na Ukoma Hospitali ya Wilaya Tunduru.
Wataalam kutoka kitengo cha Kifua Kikuu na Ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru wakitoa huduma ya uchunguzi kwa watu wa jamii ya Wafugaji wanaofanya shughuli zao katika kitongoji cha Chilundundu kata ya Misechela wilayani humo.
………………………
Na Muhidin Amri, Tunduru
WIZARA ya Afya kupitia mpango wa Taifa wa kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma imesema,kampeni ya mpango harakishi wa uibuaji Wagonjwa wa Kifua Kikuu itawafikia watu wote waliobainika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo ambao hawakufikiwa mwaka 2024.
Watu hao,wataanzishiwa Dawa haraka kwa ajili ya kuzuia uwezekano wa kuambukiza watu wengine ili kuifanya Tanzania kuwa nchi salama bila kuwa na watu walioambukizwa ugonjwa wa kifua kikuu ifikapo mwaka 2030.
Hayo yamesemwa jana na Mwakilishi wa Wizara ya Afya kitengo cha kudhibiti Kifua Kikuu na Ukoma Dkt Jacob Mwanamtwa,baada ya kukagua utekelezaji wa kampeni hiyo katika maeneo mbalimbali ya wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma.
Alisema,Wizara ya Afya imejipanga na itahakikisha inawapata wagonjwa ambao hawakupatikana mwaka 2024 na kuwaanzishia matibabu yanayotolewa bure kwenye vituo vya Afya na Hospitali zote hapa nchini.
“Wagonjwa ambao hawajapatiwa matibabu wanaendelea kuambukiza watu wengine katika jamii yetu na mbaya zaidi mgonjwa ambaye hajaanza kutumia Dawa anaweza kuambukiza watu kati ya 10 hadi 15 kwa mwaka”alisema Dkt Jacob.
Alisema,wameanza kampeni hiyo kwenye mikoa tisa hapa nchini ambayo haikufanya vizuri katika kuibua wagonjwa wa kifua kikuu mwaka jana ikiwemo Mkoa wa Ruvuma na kupitia kampeni hiyo wagonjwa wote watafikiwa ili waweze kuanzishiwa matibabu.
Alisema,malengo ya Shirika la Afya Duniani(WHO) kutokomeza ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030, lakini kutokana na changamoto mbalimbali yanaweza yasifikiwe au yakafanikiwa kutokana na mikakati iliyowekwa na Serikali yetu kupitia Wizara ya Afya.
Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma wa Wilaya ya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema,kupitia kampeni ya mpango harakishi watahakikisha wananchi wote wanapata elimu ya kifua kikuu,wanafanyiwa uchunguzi na ambao watabainika kuwa na vimelea vya ugonjwa huo wataanzishiwa dawa.
“katika kipindi hiki cha mpito ambacho tunatakiwa kufanya kazi kwa juhudi kubwa tumeanza kuangalia maeneo hatarishi zaidi,baada ya hapo wataalam tutasambaa kwenye maeneo mengine ambayo siyo hatarishi lakini kuna watu ambao wako kwenye hatari ya kupata ugonjwa huo”alisema Mkasange.
Mkasange ametaja maeneo hatarishi ni kwenye maboma ya wafugaji,vijiwe vya boda boda,wacheza bao,Pooltable machimbo ya madini na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu kuanzia watano na kuendelea.
Aidha alisema,kabla ya Wizara ya Afya kuzindua mpango harakishi wa kuibua wagonjwa wa TB,Wilaya ya Tunduru imeshaanza kutekeleza kampeni hiyo kwenye vijiji vyote vinavyozungukwa na machimbo ya madini,shule za Msingi na Sekondari za bweni.
Mkasange alisema,walianza kampeni ya uelimishaji,uibuaji na uchunguzi wa TB mapema ili kwenda na kasi ya mpango harakishi wa uibuaji Wagonjwa wa Kifua Kikuu iliyozinduliwa wiki iliyopita ili kukata mnyororo wa maambukizi katika wilaya ya Tunduru.
Naye Mratibu wa huduma za maabara Mkoa wa Ruvuma Said Kaunde alisema, kampeni ya mpango harakishi ya uibuaji Wagonjwa wa Kifua Kikuu imegawanyika kwenye makundi mawili ambayo ni kuwafikia Wananchi wenye vimelea vya TB kwa ajili ya kuchukua sampuli za makohozi na kuwaanzishia Dawa.
Alisema,katika mkakati wa kutokomeza ugonjwa huo Serikali yetu imewekeza fedha nyingi kwenye vifaa tiba hasa kununua mashine za kisasa za uchunguzi wa vimelea vya kifua kikuu na katika Mkoa wa Ruvuma kuna mashine 11 ambazo zimepelekwa kwenye Halmashauri zote nane.
Pia alisema,tangu kampeni hiyo ilipoanza hadi sasa wamefanikiwa kukusanya sampuli zaidi ya 851 ambazo baada ya kupelekwa maabara kwa ajili ya uchunguzi,24 zimekutwa na maambukizi ya ugonjwa huo.
Muhudumu wa afya ngazi ya jamii Idd Yakiti(Nyuki) alisema,kwenye kampeni ya uibuaji wa Wagonjwa wa Kifua Kikuu kazi anayofanya ni kwenda kwenye zahanati ili kuchukua makohozi ya wahisiwa na kuzifikisha Hospitali ya wilaya kwa ajili ya uchunguzi.
Nyuki, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuchukua hatua katika kukabiliana na ugonjwa huo ambao ni miongoni mwa magonjwa kumi Ulimwenguni yanayoongoza kusababisha vifo vya watu wengi.