NA JOHN BUKUKU, DAR ES SALAAM
Timu ya wataalamu wa Wizara ya Afya kutoka Jamhuri ya Somalia wamewasili nchini kwa ziara ya siku saba ili kujifunza masuala mbalimbali ya kiutendaji, hususan jinsi Bohari ya Dawa (MSD) inavyosimamia usambazaji wa dawa na vifaa tiba kupitia mifumo yake ya kisasa.
Akizungumza leo Februari 3, 2025, jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Tukai Mavere, amesema kuwa ziara hiyo ni muhimu kwa ajili ya kubadilishana uzoefu, kujifunza, na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Somalia katika sekta ya afya.
Tukai amesema kuwa Rais wa Somalia alitembelea MSD mwaka 2024 na kutoa ahadi ya kuimarisha ushirikiano huo, jambo lililofanikisha ziara hii ya wataalamu wa afya kutoka Somalia. Aliongeza kuwa Desemba 2024, ujumbe kutoka Tanzania ulifanya ziara nchini Somalia kwa lengo la kuboresha mnyororo wa ugavi wa dawa na kubadilishana uzoefu wa kiutendaji.
“Tutakuwa nao kwa muda wa wiki moja, ambapo wataangalia namna tulivyofanikisha mifumo yetu ya ugavi wa dawa na vifaa tiba. MSD imepiga hatua kubwa na imekuwa mfano wa kuigwa na mataifa mengi barani Afrika,” alisema Tukai.
Aliongeza kuwa Tanzania imewekeza kwa kiwango kikubwa katika mifumo ya usimamizi wa dawa, ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa na uweledi wa wafanyakazi, hatua ambayo imeiwezesha MSD kuwa na miundombinu bora ya usambazaji wa dawa kwa hospitali, vituo vya afya, na zahanati kote nchini.
Katika kipindi cha ziara yao, viongozi hao kutoka Somalia watazuru ofisi za MSD za kanda na kukutana na wateja wake, ili kujifunza kwa kina kuhusu utendaji wa taasisi hiyo katika kusimamia upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa wakati.
Katika hatua nyingine, MSD imeendelea kuimarisha miundombinu yake ya kuhifadhi na kusambaza dawa kwa kukifanya kituo chake cha Dodoma kuwa kitovu (hub) kikuu cha usambazaji wa dawa na vifaa tiba nchini.
Ghala hilo la kisasa jijini Dodoma linajumuisha:
Eneo kubwa la kuhifadhi dawa na vifaa tiba kwa ufanisi wa hali ya juu.
Mifumo ya kisasa ya usimamizi wa ugavi, ikiwemo e-LMIS (Electronic Logistics Management Information System) kwa ufuatiliaji wa bidhaa kwa muda halisi.
Teknolojia maalum za uhifadhi wa dawa zinazohitaji ubaridi wa hali ya juu, kama chanjo na dawa za dharura.
Mifumo ya udhibiti wa joto na unyevunyevu ili kuhakikisha dawa zinakidhi viwango vya ubora kimataifa.
Kwa mujibu wa MSD, hatua hii itaongeza ufanisi wa usambazaji wa dawa, kupunguza ucheleweshaji wa bidhaa za afya, na kuboresha huduma za afya kwa wananchi kote nchini. Dodoma sasa inakuwa kitovu kikuu cha MSD, ikihudumia mikoa yote na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa dawa kwa vituo vya afya vya umma.