FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Wakazi wa Kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro, wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka kuboresha barabara ya Kilombero-Mazimbu Fam ili kukabiliana na changamoto za mafuriko yanayotokea wakati wa mvua za masika.
Wakazi hao wamesema kuwa hali ya barabara hiyo inapozidiwa na maji, mawasiliano hukatishwa kwa masaa kadhaa, hali inayosababisha maafa na kurudisha nyuma shughuli zao za kiuchumi.
Frank Alpakshard, dereva wa bajaji anaefanya shughuli ya kusafirisha abilia kutoka mjini kwenda Lukobe, ameiomba Serikali kuweka miundombinu rafiki kwenye barabara hiyo ili kuhakikisha usalama wa watumiaji na kupunguza gharama za matengenezo ya vyombo vya moto vinavyoharibika mara kwa mara kutokana na hali mbaya ya barabara.
Naye Getruda Cosmas, mkazi wa Mtaa wa Tushikamane, amesema kuwa barabara hiyo wakati wa mvua haipitiki na vyombo vya moto inawalazimu kutembea kwa miguu kwenye maji mengi, jambo linalohatarisha afya zao.
“Mvua zikianza, tunashindwa kwenda kazini kwa siku kadhaa. Hii inatupunguzia kipato na kuhatarisha maisha yetu,” amesema Getruda.
Akizungumza na Michuzi TV, Diwani wa Kata ya Lukobe, Selestine Mbilinyi, ametoa wito kwa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuharakisha ujenzi wa barabara hiyo kabla ya madhara zaidi kujitokeza.
“Tusisubiri kuona madaraja na vivuko vinaharibiwa na mafuriko ndipo tuchukue hatua. Ni muhimu hatua zichukuliwe mapema ili kuokoa maisha na mali za wananchi,” amesema Mbilinyi.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Emmanuel Ndyamukama, amethibitisha kuwa Serikali tayari imeanza usanifu wa barabara hiyo, na mara baada ya usanifu kukamilika, barabara itajengwa kwa kiwango cha lami. “Tutazingatia vigezo vya ujenzi wa eneo lenye maji ili kuhakikisha barabara inakuwa salama na ya kudumu. Hii itasaidia pia kudhibiti maji mengi yanayotoka kutoka maeneo na wilaya jirani,” amesema Mhandisi Ndyamukama.
Kwa mujibu wa kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoa wa Morogoro, mafuriko yaliyotokea mwezi Januari 2024 yalisababisha vifo vya watu 30, jambo linaloonesha ukubwa wa tatizo hilo na umuhimu wa kuchukua hatua za haraka.
Wananchi wana matumaini kuwa Serikali itachukua hatua stahiki ili kuhakikisha usalama wa maisha na mali zao unalindwa wakati wa mvua zijazo