Fundi anayejenga mradi wa maji wa Kilindi-Barabara kata ya Matiri Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Stanley Mlelwa wa pili kushoto akimuonyesha Mwenyekiti wa kijiji cha Barabara Ebhati Kapinga wa pili kulia,maji ya bomba yatakayosambazwa kwa Wakazi wa kijiji na Kilindi wapatao zaidi ya 3,800 ambao tangu Uhuru hawajawahi kupata maji ya bomba,kulia Afisa Uhusiano wa Ruwasa Mkoa wa Ruvuma Geddy Ndimbo(Picha na Muhidin Amri).
Fundi anayejenga mradi wa maji wa Kilindi-Barabara kata ya Matiri Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Stanley Mlelwa wa pili kushoto,na Afisa Uhusiano wa Ruwasa Mkoa wa Ruvuma Geddy Ndimbo kulia,wakimsikiliza Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Barabara kata ya Matiri Halmashauri ya Wilaya Mbinga Mkoani Ruvuma Ebhati Kapinga wa pili kulia,baada ya Serikali kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(Ruwasa) kuanza kutekeleza mradi wa maji ya bomba utakaonufaisha Wakazi wa kijiji hicho na Kilindi.
Baadhi ya mabomba yatakayotumika kusambaza maji safi na salama kwa Wakazi wa kijiji cha Barabara kama yanavyoonekana.
……….
Na Muhidin Amri, Mbinga
WAKALA wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini(RUWASA)Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma,upo katika hatua za mwisho kukamilisha ujenzi wa mradi wa maji wa Kilindi-Barabara unaotarajiwa kumaliza kabisa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Wanufaika wa mradi huo ni Wananchi zaidi ya 3,800 wa Kijiji cha Kilindi na Barabara,ambao kwa muda mrefu hawana huduma ya maji ya uhakika, badala yake wanatumia maji kutoka kwenye visima vya asili,mito na mabonde.
Meneja wa RUWASA Wilayani Mbinga Mashaka Sinkala alisema,mradi huo unatekelezwa kwa kutumia mafundi wa ndani na utakamilika mwishoni mwa mwezi huu na gharama za ujenzi wake ni Sh.milioni 68.
Akizungumzia kuhusu miradi ya program ya uchimbaji visima 900/5 kwa kila Jimbo Sinkala alisema,wanatekeleza kwa kuboresha chemchem za asili zilizopo kwani Jiografia ya Mbinga hairuhusu kuchimba visima na tayari wameanza kwenye vijiji vinane na vijiji viwili wako kwenye hatua ya manunuzi.
Kwa mujibu wa Sinkala,miradi hiyo itakapokamilika itawanufaisha watu 11,700 na kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa asilimia 3.1 hivyo kupanda kutoka asilimia 70 hadi kufikia asilimia 74 na vijiji vitakavyopata huduma ya maji kuongezeka kutoka 107 hadi 117.
“Miradi hii inayoendelea kutekelezwa katika Wilaya yetu ya Mbinga itagharimu Sh.milioni 470,itakuwa na manufaa makubwa kwa kuboresha maisha ya Wananchi na kupunguza tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji katika vijiji husika”alisema Sinkala.
Aidha,ametaja mradi mwingine ni mradi wa maji Kindimbachini unaotekelezwa kwa gharama ya Sh.milioni 48 na uko hatua za mwisho ya kukamilika ambapo,ameipongeza Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji ambayo itamaliza changamoto ya maji safi na salama kwa Wananchi wa Mbinga.
Fundi anayejenga mradi wa maji Kilindi-Barabara Stanley Mlelwa,ametaja kazi zilizofanyika ni kutoa maji kwenye chanzo hadi kwenye eneo litakalojengwa tenki umbali wa kilometa 3.6,kuchimba mitaro na kulaza mabomba.
Ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kupeleka miradi hiyo vijijini kwani inawaondolea Wananchi changamoto ya huduma ya maji na baadhi ya vijana wenye ujuzi kupata kazi zinazowaingizia kipato.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Barabara Ebhati Kapinga,alieleza kuwa ni faraja kubwa kuona Serikali ya awamu ya sita inatekeleza kwa vitendo Kauli yake ya kumtua Mama ndoo kichwani ambayo imewezesha vijiji mbalimbali ikiwemo kijiji cha Barabara kupata mradi wa maji ya bomba.
Alisema, kwa muda mrefu wanawake na watoto wa kijiji hicho wanateseka kwa kubeba ndoo za maji kichwani kutoka mtoni hadi majumbani,hivyo mradi huo utawaondolea mateso na kuboresha maisha yao kwa kujenga nyumba bora na kupata muda mwingi wa kujikita kwenye shughuli za uzalishaji mali.
Kapinga alisema,Serikali ya kijiji na Wananchi watahakikisha wanalinda mradi huo ili uweze kuwa endelevu,kwa kuwa wamechoka kutembea umbali mrefu kila siku kwenda kutafuta maji kwenye mito na vyanzo vingine vya asili ambavyo maji yake siyo safi na salama.
Mkazi wa kijiji hicho John Ndimbo alisema,changamoto ya maji katika kijiji hicho ni ya muda mrefu,hata hivyo ameiomba Serikali kupitia RUWASA kukamilisha mradi huo haraka ili waweze kupata huduma ya maji ya uhakika.