Na. Samson Samson, Njombe
Kutokana na serikali kutumia mfumo wa NeST katika kuomba Zabuni za miradi mbalimbali, imeelezwa kuwa mfumo huo umekuwa ni changamoto kupata wazabuni kwa wakati sambamba na kutokuwa na ukomo wa muda wa ukamilishaji mradi.
Akisoma taarifa ya mradi wa shule mpya ya sekondari Chief Dastan Masasi iliyopo katika kata ya Masasi,mbele ya kamati ya siasa Wilaya ya Ludewa katibu wa mradi huo Januar Chaula amesema katika mradi huo kuna baadhi ya zabuni zimekosa wazabuni licha ya kurudia rudia matangazo huku zilizopata wazabuni wakichukua muda mrefu kuleta vifaa eneo la mradi,hali ambayo imesababisha kukwama kwa mradi.
” Hapa tumetangaza zabuni za ‘frem’ na milango toka mwezi Novemba, 2024 lakini hadi sasa hakuna mzabuni aliyeomba zabuni hii”.
Mradi huo unaogharimu kiasi cha zaidi ya Sh. Mil. 583. 8 mpaka sasa umefikia 85% ya ukamilikaji wake na tayari umekwisha tumia kiasi cha Sh. Mil. 368.7 huku nguvu za wananchi ikiwa ni kiasi cha Sh. Mil. 45,000,000.
Aidha akizungumza kwa niaba ya kamati ya siasa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Wilaya ya Ludewa Stanley Kolimba amepongeza hatua iliyofikiwa katika mradi huo huku akiwataka wasimamizi wa mradi huo kuongeza spidi ya ujenzi wake licha ya kukabiliana na changamoto za wazabuni ili wanafunzi wanaotoka katani hapo na kutembea umbali zaidi ya KM. 15 Kufuata huduma ya elimu waweze kuhamishiwa katika shule hiyo na kupata elimu jirani.
Kamati hiyo ya siasa ambayo inafanya ziara ya siku mbili ambapo kwa siku ya kwanza imetembelea miradi mitano ambayo ni mradi wa Maji kitongoji cha Mdonga, Mradi wa kilimo wa kikundi cha vijana Lifua, Kituo cha Afya Luilo, Zahanati ya Lihagule, pamoja na shule ya Sekondari Masasi.