Tanzania
Mortgage Refinance Company Limited (TMRC) leo imeikaribisha Benki ya
KCB Tanzania Limited kama mwanahisa wake mpya. Benki ya KCB Tanzania
Limited imejiunga na TMRC kama mbia wa 20 kufuatia uwekezaji wa mtaji wa
TZS 500 milioni katika TMRC.
Uwekezaji huu wa Benki ya KCB
katika TMRC ulihitimishwa Desemba 2024. KCB Bank inaungana na wanahisa
wengine wa TMRC wa taasisi za fedha ikiwa ni pamoja na CRDB Bank Plc;
Benki ya NMB Plc; Benki ya Taifa ya Biashara (NBC); TIB Development Ltd;
Azania Bank Plc; Exim Bank (T) Ltd na DCB Commercial Bank Plc. Wanahisa
wengine wa TMRC wa taasisi za fedha ni pamoja na Access Bank Ltd; Benki
ya Afrika (T) Ltd (BOA); First Housing Finance Ltd; Peoples Bank of
Zanzibar Ltd (PBZ); I&M Bank (T) Ltd; NCBA Bank Ltd , Mkombozi
Commercial Bank Plc na Mwanga Hakika Bank(MHB).
Umiliki wa hisa
wa TMRC unajumuisha Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Taasisi za Fedha
za Maendeleo ya Kimataifa (DFIs) kama vile Shelter Afrique (taasisi ya
kifedha ya Kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika) na Shirika la Fedha la
Kimataifa (IFC) ambalo ni sehemu ya Kundi la Benki ya Dunia.
Kwa
hatua ya Benki ya KCB kujiunga na TMRC, inamaanisha benki hiyo itaweza
kupata fedha nyingi zaidi kwa madhumuni ya mikopo ya nyumba kutoka TMRC
kama sehemu ya mkakati wake wa kukuza biashara yake kupitia utoaji wa
mikopo ya nyumba.
Akizungumza wakati wa mkutano na wanahabari,
Mkurugenzi wa Biashara wa Kanda wa KCB Group na Mkurugenzi Mtendaji wa
Benki ya KCB Tanzania, Bw. Cosmas Kimario, alisema hatua hiyo itaongeza
tija katika kuimarisha ukwasi ili kupanua wigo wa huduma za mikopo ya
nyumba inayotolewa na benki hiyo hapa nchini.
“Kwa miaka mingi,
KCB Bank Tanzania imekuwa mshirika wa kuaminika katika sekta ya mikopo
ya nyumba, ikitoa suluhisho bunifu za kifedha zinazowawezesha watanzania
wengi kumiliki makazi yao. Kupitia uwekezaji huu, tunajizatiti zaidi
katika kusaidia maendeleo ya sekta ya nyumba kwa kuleta suluhisho
endelevu na kuongeza fursa za ujenzi wa nyumba nchini,” alisema.
Aliongeza
kuwa, kwa kujiunga na kuwa mwanahisa wa TMRC, inamaanisha kikomo cha
ufadhili wa fedha wa muda mrefu kwa benki hiyo kutoka TMRC kitaongeza
hadi Sh10 bilioni ikiwa ni mara ishirini ya uwekezaji huo.
“Hii
inamaanisha kwamba benki ya KCB itapata kuwa na fedha zaidi ambazo
zitaelekezwa kwenye mikopo ya nyumba kwa wateja wetu ili kukidhi
mahitaji ya soko ya sasa ya mikopo ya nyumba na kutatua changamoto ya
uhaba wa nyumba za makazi unaokabili taifa letu,” alisema.
Kufikia
Septemba 2024, KCB Bank ilishika nafasi ya nane (8) katika sekta ya
benki kwa mujibu wa ripoti ya BOT, ikitoa mikopo yenye thamani ya TZS
34.1 bilioni na kushikilia sehemu ya soko ya (market share) 4.75%, huku
wateja 175 wakinufaika na mikopo hiyo.
Kufikia Desemba 2024,
thamani ya mikopo iliyotolewa na KCB iliongezeka hadi TZS 34.6 bilioni
ikijumuisha mkopo wa Sh10 bilioni kutoka TMRC, ambapo kati ya wateja
175, takriban 99 walifaidika kupitia fedha hizo za TMRC.
Cosmas Kimario- Group Director of Regional Businesses & Managing Director KCB Tanzania Limited
Oscar Mgaya -Chief Executive Officer of Tanzania Mortgage Refinance Company (TMRC)